Vigogo Kuondolewa kwa Nguvu nyumba za Serikali
VIGOGO wakiwamo wabunge na wananchi wengine, walionunua nyumba za serikali na kutomaliza kulipa madeni yao kwa wakati kama mikataba yao inavyoelekeza, wameanza kuondolewa kwa nguvu kwenye nyumba hizo na nyumba kupigwa mnada ili kupata fedha za kulipa madeni ya Sh bilioni sita.
Madeni hayo serikali inadai kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yono Auction Mart ambayo imepewa kazi ya kukusanya madeni hayo ya TBA kutoka kwa wadaiwa sugu hao, Scholastica Kevela alisema kazi ya kuwaondoa vigogo walionunua nyumba hizo au kupangisha bila kulipa, inaanza leo jijini Dar es Salaam.
Kevela alisema katika kazi hiyo, TBA wamewapa orodha ya zaidi ya nyumba 3,000 nchi mzima za walionunua na wengine kupangisha nyumba za TBA ambao wanadaiwa madeni na muda wa kurejesha ulishapita.
“Tuna orodha za nyumba zaidi ya 3,000 nchi nzima, juzi tulianza Mwanza tumeshikilia nyumba zaidi ya 20, kwa kuwatoa watu nje, na juzi Dodoma tumefanya hivyo, tumeshashikilia nyumba 40 zikiwemo za vigogo, kesho (leo), tunaanza zoezi hilo hapa Dar, hatutakuwa na huruma kwa mdaiwa, wote tulishawapa taarifa za kimaandishi, kazi yetu ni utekelezaji tu,” alisema Kevela.
Alisema wanatekeleza kazi waliyopewa kwa sababu hata Rais John Magufuli anasisitiza wananchi kulipa kodi ili nchi iendelee na kuacha utegemezi, hivyo wadaiwa sugu hao muda wa kulipa na hata muda wa ziada waliopewa kuhakikisha wamemaliza madeni yao nao ulipita na wengi hawakulipa, hivyo Yono inaingia kazini kupiga mnada nyumba hizo.
Alisema walionunua nyumba za serikali na hawajamaliza kulipa madeni wakiwemo wabunge, vigogo na wananchi wengine wanajitambua, hivyo kuanzia leo wanapaswa kuondoka kwani zitauzwa ili kulipa deni la serikali.
Kadhalika alisema waliopanga kwenye nyumba hizo na bado wanadaiwa kodi msako huo unawahusu na kwamba wataondolewa wote na vitu vyao kupigwa mnada ili kupata fedha za kulipa kodi wanayodaiwa na serikali.
“Sisi tunatekeleza agizo kulingana na mkataba wetu na pia tunamsaidia Rais kukusanya kodi, hivyo wote wanaodaiwa wafahamu tutawafuata walipo na kupiga mnada mali zao ili kulipa kodi ya serikali,” alisema Kevela.
Hata hivyo, alisema mchanganuo wa nyumba hizo na majina ya vigogo na wabunge watatoa baadaye baada ya kufanya upembuzi kwa sababu nyumba za wadaiwa ni nyingi.
Awali akizungumzia madeni ya wakwepa kodi wa Mamlaka ya Mapato (TRA), waliokwepa kulipia kontena zaidi ya 320 zilizogunduliwa na Rais Magufuli, Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni hiyo, Yono Kevela alisema wanaendelea kukusanya madeni ya wadaiwa hao.
Alisema Yono imekamata mali za wadaiwa hao na baadhi zimeshapigwa mnada na nyingine zinaendelea kuuzwa ili kupata fedha za kulipa kodi, na hadi sasa takribani Sh bilioni saba zimeshalipwa kati ya Sh bilioni 18 zilizokuwa zinadaiwa.
Post a Comment