Serikali Yafuta Adhabu ya Jela Kuhusu Kutodai Risiti
Waziri wa Fedha na Mipango nchini, Dkt. Philip Mpango, amefafanua adhabu ya kosa la kutotoa ama kudai risiti katika manunuzi na kusema kuwa serikali imefuta kipengele cha kufungwa na pia faini itatozwa kulingana na ghamara ya bidhaa itakayonunuliwa.
Akizungumza leo Mjini Dodoma na kupitia Shirika la Habari la Taifa, Dkt. Mpango amesema kuwa wameamua kufanyia marekebisho sheria hiyo kutokana na maoni ya wadau mbalimbali lakini bado adhabu itatolewa kwa mtu yeyote asietoa ama kudai risiti wakati wa mauzo.
Dkt. Mpango amesema kuwa moja kati ya faida kwa wafanyabishara katika kutoa risiti ni pamoja na kuweka rekodi nzuri katika biashara lakini pia na mnunuzi kujua ni kiasi gani umekatwa kwa ajili ya kodi.
Amesema kuwa sheria waliyoiweka sasa adhabu itatolewa kutokana na ukubwa wa mauzo ya mfanyabiashara ili kuwalinda wafanyabiashara wadogo ambao watakuwa wanatenda makosa hayo ili kuwakumbusha umuhimu wa kutoa risiti katika mauzo yao.
Ameeleza kuwa lengo kuu la kufanya hivyo ni kujenga taifa lenye utamaduni wa kulipa kodi lakini pia fedha hizo zitasaidia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo katika sekta ya Afya, Elimu na maeneo mengine.
Dkt. Mpango amesema kuwa wapo wafanyabiashara wengine wanauza mamilioni ya shilingi lakini hawatoi risiti za mauzo yao jambo ambalo linaikosesha serikali mapato halali na pia mnunuaji anakua hajui ni kiasi gani cha kodi amekatwa kutoka na manunuzi ya bidhaa hizo.
Post a Comment