Serikali Mbioni Kufungua Ubalozi mpya Qatar
TANZANIA inatarajia kufungua ubalozi wake nchini Qatar kwa lengo la kuendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizo huku ikitilia mkazo katika sekta za gesi asilia, utalii, usafiri wa anga na mawasiliano.
Rais, Dk John Magufuli alisema hayo jana Ikulu, Dar es Salaam alipokutana na kuzungumza na Balozi wa Qatar nchini, Abdallah Jassim Al Maadadi.
Pamoja na kutangaza kuufungua ubalozi wake nchini Qatar, Magufuli amemuomba balozi huyo kufikisha ujumbe kwa Kiongozi wa Qatar, Shehe Tamim bin Hamad Al Thani na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Qatar kwamba zipo fursa nyingi za ushirikiano zinazoweza kufanyiwa kazi, huku akibainisha uwepo wa gesi asilia zaidi ya futi za ujazo trilioni 57 na mpango wa kufufua Kampuni ya Ndege ya Taifa (ATCL).
“Najua Qatar ina uzoefu katika maeneo hayo na sisi Tanzania tungependa tushirikiane nanyi kuwekeza na kubadilishana uzoefu ili fursa hizo zilete manufaa kwa pande zote mbili,” alisema Rais Magufuli.
Naye Balozi Al Maadadi alimshukuru Rais Magufuli kwa nia yake ya kufungua Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar na kuimarisha zaidi ushirikiano na uhusiano na nchi hiyo, na ameahidi kufikisha ujumbe kwa kiongozi wa Qatar na jumuiya ya wafanyabiashara Qatar waje kuwekeza Tanzania.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kuzungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambaye pia Spika mstaafu wa Bunge, Anne Makinda, Ikulu, Dar es Salaam.
Baada ya mazungumzo hayo, Makinda alisema mazungumzo yao yameihusu NHIF na kwamba amemhakikishia kuwa amejipanga kuona mfuko huo uliobeba matumaini ya huduma za matibabu ya Watanzania unaboreshwa zaidi na dosari zinazolalamikiwa na wanachama zinafanyiwa kazi.
Post a Comment