Header Ads

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete Ateuliwa Kuwa Balozi wa Heshima


KITUO cha Ufundi cha Kilimo na Maendeleo Vijijini (Technical Centre for Agricultural and Rural Cooperation, CTA) kilicho chini ya Umoja wa Ulaya (EU) chenye makao makuu mjini Wageningen, Uholanzi kimemteua Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete kuwa Balozi wa Heshima (Goodwill Ambassador) wa Maendeleo ya Kilimo katika Mabara ya Afrika, Karibiani na Pacific.

Katika barua iliyokabidhiwa na mjumbe wa Bodi ya CTA, Prof. Faustin Kamuzora, CTA wameainisha kuwa Dk. Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, ameteuliwa kwa kutambua mchango na juhudi zake katika kukiendeleza kilimo nchini Tanzania na barani Afrika.

Katika wadhifa wake huo mpya, CTA imemuomba Dk. Kikwete aweze kuiwakilisha katika makongamano ya kimataifa ambapo atazungumzia umuhimu wa kukiendeleza kilimo kwa ajili ya kutoa fursa ya ajira zenye staha na uhakika kwa vijana na wanawake katika nchi za barani Afrika, Karibiani na Pasifiki. Pia ataisaidia CTA katika kuandaa makala na kufanya mahojiano na waandishi wa habari katika nchi mbalimbali.

Dk. Kikwete amekubali uteuzi huo na kuahidi kushirikiana na CTA katika kutekeleza mambo ambayo ameombwa kusaidiana na taasisi hiyo ambayo ni ya ushirikiano wa Umoja wa Ulaya na Kundi la nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki wenye makao makuu mjini Brussels, Ubelgiji.

Prof. Kamuzora ambaye pia ni Katibu Mkuu, Mawasiliano ni mjumbe wa Bodi ya CTA akiwakilisha nchi za ukanda wa Afrika Mashariki kwa miaka mitano tangu 2013 hadi 2018.

No comments