Header Ads

Nape: CCM Imejaa Majipu


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amesema ndani ya chama hicho tawala kuna majipu mengi yanayohitaji kutumbuliwa. 

Kwa mujibu wa katibu huyo wa uenezi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi, hatua hiyo ndiyo njia pekee ya kuleta mapinduzi na mageuzi ndani ya chama hicho. 

Amesema chama hicho kilishaingiliwa na makolokolo, hivyo yanahitaji kusafishwa yote kwa mustakabali wake. 

Kauli ya Nape ni sawa na ile iliyowahi kutolewa na viongozi wakuu wa nchi. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan mwanzoni mwa mwaka huu akiwa mkoani Tanga alisema ndani ya CCM kuna watu majipu ambao wameficha makucha ili wasijulikane uovu wao. 

Siku ambayo Rais John Magufuli alipewa cheti na Tume ya Uchaguzi (NEC) baada ya kushinda uchaguzi alikwenda kwenye ofisi ndogo za CCM Lumumba na kuhutubia huku akisisitiza kuwa ndani ya chama hicho kuna watu wanafiki. 

Nape anasema pamoja na kutumbua majipu, chama hicho pia kinahitaji kujitathimini muundo wake kwa kuwa uliopo sasa ni mkubwa na hauendani na hali halisi ya kipato cha chama.

“Muundo wetu ni mzigo mzito unaongeza urasimu. Kwa mfano wajumbe wa NEC hivi sasa wapo zaidi ya 400 ni mzigo mkubwa kwa chama matokeo yake walitumia fursa kutafuta ubunge, inahitaji marekebisho makubwa kwa kuwa uchumi wa chama ni mdogo kwa sasa, tunategemea ruzuku tu. "- Nape

Alisema hata katika upande wa watumishi wa chama wapo wengi sana na wote si wanasiasa, robo tu ndiyo wanasiasa.

Kwa mujibu wa Nape, kwa sasa kinachohitajika ni kutengeneza chama kidogo ili gharama ya kuendesha iwe ndogo. 

Alisema sababu nyingine ya kusafisha chama kutokana na urasimu uliopo; “Lazima tupunguze mlolongo wa vikao vya kutoa maamuzi lakini pia tuangalie upya sera na taratibu zetu.” 


 Akizungumzia watu wenye tabia ya kuhama vyama kama ilivyotokea kwa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa na kundi lake, Nape alisema yeye si muumini wa hilo.

“Mimi siamini katika kuhama  vyama ni sawa na kumsilimisha Papa. Kwangu kuchukua watu kutoka upinzani ni sawa na gari zima kuwekewa vifaa chakavu. Watanzania waliopo katika vyama vya siasa hawazidi milioni 10 kwa nini tunyang’anyane wakati kuna zaidi ya watu milioni 45."- Nape


Akizungumzia utendaji wa Rais John Magufuli, Katibu huyo wa uenezi wa chama hicho anayetarajia kustaafu hivi karibuni katika mkutano mkuu alisema ameanza vizuri na kwamba mtindo wake wa kutumbua majipu ndiyo hasa ulikuwa ufanyike baada ya wananchi kukosa imani na Serikali kwa muda mrefu.

 “Yanayotekelezwa hivi sasa na Rais Magufuli ni ripoti yetu. Baada ya kuzunguka nchi nzima tuligundua mambo mengi na ili kukiweka salama chama hatuna budi kuhakikisha tunasafisha uozo wote. 

“Ilifika wakati wawekezaji wamechukua ardhi hawaitumii, wananchi hawana ardhi tena matokeo yake ni migogoro kila kukicha, walimu wanadai haki yao watu wenye mamlaka hawatimizi wajibu wao matokeo yake kukaanza kujengeka hisia kwamba walimu ni wapinzani.

 "Hivi mtu anakuwaje mpinzani kama anadai haki yake? Mlipe kwanza haki yake uone kama ataendelea na malalamiko,” alisisitiza Nape ambaye aliingia rasmi katika siasa akiwa kijana mdogo wa miaka 20 tu. 

Alisema Rais Magufuli amerejesha heshima kwani nchi ilifika mahali ambapo wezi wa mali ya umma walionekana ndiyo wajanja na wale ambao walikuwa wana maadili walionekana legelege. 

Alisema jamii ilipotea na Taifa lilikuwa likijenga jamii ya ajabu ya watu mafisadi, wezi na wasioogopa mali ya umma na hawakuwa na wa kuwazuia kufanya wanavyotaka. 

 Akizungumzia mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya chama chake uliofanyika mkoani Dodoma mwishoni mwa mwaka jana Nape alisema vikao vilikuwa vya moto sana. 

“Wakati mwingine tulikaa katika mkutano mpaka saa tisa usiku na hata mkitoka hamtazamani usoni kila mmoja anaingia katika gari na kuondoka, palichemka sana.” 

Hata hivyo, Nape alisema anashukuru Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Jakaya Kikwete kwa kuwa na kifua na hiyo ndiyo siri ya kufanikisha mchakato huo. 

Alisema Kikwete ni mtoto wa CCM hivyo ilikuwa rahisi kumkata yeyote kwani uzoefu wake ndani ya chama ulisaidia na kwamba itachukua muda mrefu kupata kiongozi kama yeye lakini pia hawawezi kupuuza kazi iliyofanywa na Katibu Mkuu wa chama hicho Abdulrahman Kinana. 

“Ukongwe ulituvusha lakini pia wazee wakarekebisha mambo tukavuka salama, hali ilikuwa mbaya lakini ndiyo demokrasia,” alisisitiza Nape ambaye ni mtoto wa mwanasiasa mkongwe, marehemu Moses Nnauye. CCM itafanya mkutano mkuu Julai 23 mwaka huu.

No comments