Mtanzania Mwingine Akamatwa kwa Kumtukana Rais Kupitia "WhatsApp"
Mkazi wa Dar es Salaam, Leornad Kyaruzi amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shtaka la kutoa lugha ya kumdhalilisha Rais John Magufuli.
Kyaruzi alifikishwa katika Mahakama hiyo na kusomewa shtaka linalomkabili mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Magreth Bankika.
Akisoma hati ya mashtaka, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Wankyo Simon alidai mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Juni 2, mwaka huu katika jengo la Tanzania Tower lililopo Barabara ya Sam Nujoma.
Mwendesha mashtaka huyo alidai siku hiyo, mshtakiwa aliandika kupitia simu yake ya mkononi ujumbe wenye lugha ya kumdhalilisha Rais Magufuli na kisha kuusambaza kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp wakati akijua kuwa ni kinyume cha sheria.
Mshtakiwa alikana shtaka hilo na Hakimu Bankika alimtaka kuwa na mdhamimi mmoja kutoka taasisi inayotambuliwa kisheria ambaye atasaini dhamana ya Sh5 milioni na kufanikiwa kutimiza sharti hilo, hivyo kuachiwa kwa dhamana.
Awali, upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakalika na kuiomba Mahakama kupanga tarehe nyingine. Hakimu Bankika aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 18, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.
Wakati huohuo, kitendo cha baadhi ya wadau kumchangia Issack Habakuki aliyepatikana na hatia ya kumtukana Rais Magufuli mkoani Arusha, kilitinga bungeni baada ya wabunge kuitaka Serikali kutoa maelezo ya kina iwapo hakimdhalilishi kiongozi huyo wa juu nchini.
Mwongozi huo uliombwa na Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia akimtaka Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe atolee ufafanuzi jambo hilo.
Mahakama mkoani Arusha ilimtia hatiani kijana huyo mapema mwezi huu kwa kumtukana Rais katika ukurasa wake wa Facebook na kumhukumu kulipa faini ya Sh7 milioni au kwenda jela miaka mitatu na wiki iliyopita, wakazi wa Arusha walimchangia Sh4.5 milioni kukamilisha faini hiyo.
Waziri Dk Mwakyembe alisema suala hilo ni zito linalomgusa Rais na kuomba Naibu Spika Dk Tulia Ackson kumruhusu kwenda kufanya mashauriano na kumpa nafasi ya kuja kutoa msimamo wa Serikali katika mkutano huu unaomalizika Julai Mosi.
Post a Comment