Header Ads

Madini ya Helium Yagundulika Nchini


TANZANA kwa sasa inajikita zaidi katika utafiti wa madini yanayohitajika zaidi duniani yakiwemo yanayotumika kutengeneza vifaa vya simu na betri za magari, Bunge linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma limeambiwa.

Aidha katika juhudi hizo, madini aina ya helium (he) yanayotumika kwa ajili ya mitambo ya Apollo na pia kutumika kwenye vifaa vya matibabu kama MRI na NMR yamegundulika kuwepo nchini Tanzania.

Akijibu maswali ya wabunge jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema kwamba baadhi ya madini kama chuma na shaba, uhitajikaji wake duniani umepungua sana kwa sasa.

Katika maswali yao, Mbunge wa Igunga (CCM), Dalaly Kafumu alitaka kuthibitishiwa kuhusu uwepo wa taarifa kwamba utafiti wa madini nchini mwetu umepungua sana.

Akijibu swali hilo, Profesa Muhongo alitoa ufafanuzi kwamba madini yamekuwa yakitafutwa kwa vipindi na yanapokuwa mengi, uhitajikaji wake hupungua sambamba na utafiti.

Alifafanua kwamba katika miaka hii uhitaji wa baadhi ya madini kama shaba na chuma umepungua sana.

“Ndio maana utaona hata uchumi wa Zambia umeyumba kwa sababu China ambayo ndio mnunuzi mkubwa wa shaba kutoka nchini humo imepunguza mahitaji ya madini hayo,” alisema Muhongo.

Alisema madini yanayotengeza vifaa vya simu (rare earth mineral) na yale yanayotengeza betri (graphite) yataendelea kutafutwa kila mara kutokana na uhitajikaji wake na ndio maana akasema Tanzania nayo inajikita zaidi katika kusaka madini hayo.

Alifafanua kwamba madini hayo yanayotengeneza betri za magari yataendelea kuhitajika sana kwa sababu ulimwengu wa sasa unajikita zaidi katika kutengeneza magari yanayotumia umeme kwa wingi.

Kuhusu madini ya helium ambayo huwa katika mfumo wa gesi inayopatikana katika kina kifupi, Waziri Muhongo alifafanua kwamba utafiti ulifanywa na vyuo vikuu vya Oxford na Durham ulithibitisha kwamba kuna madini hayo nchini.

Alifafanua kwamba kiwango kilichogunduliwa cha madini hayo katika Ziwa Rukwa ni mita za ujazo bilioni 52.2 na kwamba utafiti zaidi unaendelea. Kwa sasa nchi inayozalisha kwa wingi madini hayo ni Marekani ambako hata hivyo, Profesa Muhongo, alisema yamekuwa yakipungua siku hata siku.

No comments