Header Ads

Lowassa Amwandikia Waraka Mzito Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu


WAZIRI Mkuu wa zamani na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema kwa mwamvuli wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amemwandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi   (IGP), Ernest Mangu.

Katika barua hiyo, Lowassa  amehoji hatua ya Jeshi la Polisi kupiga marufuku mikutano na maandamano kwa vyama vya siasa vya upinzani nchini.

Katika barua yake hiyo ya jana, Lowassa  alisema amelazimika kuchukua hatua hiyo kwa vile  wakati agizo hilo la  kupiga marufuku   mikutano inatolewa, alikuwa nje ya nchi ingawa alifikisha ujumbe na Watanzania wenye nia njema wa ndani na nje kuhusu hatua hiyo ya polisi.

“Kwanza niwie radhi kwamba nimelazimika kwa nafasi yako na yangu, kukiuka taratibu za itifaki hata nikalazimika kuandika waraka huu kwako.

“Ninafanya hivyo si kwa sababu yoyote, bali kwa sababu tu jambo au mambo yaliyonisukuma kukufikishia ujumbe huu yana uzito mkubwa na kimsingi yanaweza kuathiri mustakabali mwema wa taifa.

“IGP, siyo desturi yangu kuandika waraka wa namna hii mtandaoni au kupitia vyombo vya habari, ingawa safari hii nimelazimika kufanya hivyo   kuweka rekodi sahihi,   na kukosoa sababu ulizotoa kuwa nyuma ya agizo lako hilo,” alisema Lowassa.

Alisema wakati akiwa anatafakari kwa mshangao agizo hilo na baada ya kurejea nchini, alipigwa na butwaa zaidi baada ya kusikia Jeshi la Polisi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, limewazuia viongozi wao taifa wa vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara.

“Agizo hilo lilifuatiwa na tukio la kukamatwa, kushikiliwa na kuhojiwa kwa viongozi hao, akiwamo Mwenyekiti wetu, Freeman Mbowe huko Mwanza hivi majuzi.

“Katika matukio hayo yote, polisi mnadai kuwa na taarifa za intelijensia ambazo zinaonyesha kuwapo  uwezekano wa kutokea  vurugu kwenye mikutano hiyo ya hadhara ya vyama vya siasa,” alisema.

Lowassa  alisema madai hayo ya polisi hata IGP Mangu, aliwahi  kuyatoa awali kutokana na sababu wanazozijua wao wenyewe kama njia ya kuminya haki za msingi za katiba za vyama vya siasa kujumuika na kutimiza majukumu yao ya siasa.

“Si hivyo tu, uzoefu wa historia unakinzana na kwenda kinyume kabisa na madai hayo, kwa sababu  yako matukio mengi ambayo yamethibitisha kwamba mijumuiko ya wanasiasa wa vyama vya upinzani, yakiwamo maandamano na hata mikutano, imekuwa ikifanyika kwa amani.

“Iko mifano mingi inayoonyesha kwamba  tumefanya shughuli mbalimbali za siasa kwa maana ya maandamano na mikutano yahadhara kwa amani na pasipo kuwapo hata   ulinzi wa polisi.

“…Mifano ya namna hiyo ndiyo inayosababisha baadhi yetu si tu tupingane na maagizo yanayotoa mwelekeo wa kukandamizwa   uhuru wa  katiba wa vyama vya siasa vya upinzani kujumuika, bali kwenda mbali zaidi na kutilia shaka hata maagizo hayo na kuyaona kuwa na misukumo iliyojificha nyuma ya kichaka cha ‘sababu za intelejensia,”alisema.

Alisema anaandika barua hiyo aliyoiita waraka kwa mkuu huyo wa polisi kwa dhati   kwamba,  kilichotokea Kenya hivi karibuni ambako mahakama ilitupilia mbali maagizo ya namna hiyo ya polisi kujaribu kuzuia haki ya katiba ya vyama vya upinzani kuandamana ndicho kinachoelekea kutokea hapa nchini.

No comments