Kanali Feki Atapeli Vijana 62 Kwenda Jeshini
Mmoja wawaliotapeliwa.
DAR ES SALAAM: Kundi la vijana zaidi ya 62 kutoka Mikoa ya Njombe, Mbeya na Iringa wameingizwa mkenge na mtu ambaye jina lake halijafahamika mara moja, aliyejipa cheo cha ukanali kwenye Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), aliyewaahidi kuwafanyia mpango wa kujiunga na jeshi hilo baada ya kila mmoja wao kutoa shilingi 200,000.
Akizungumza na gazeti hili Ijumaa iliyopita juu ya tukio hilo, Kamishna Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, Abdulkarim Shah akiwa ofisini kwake Makao Makuu ya Skauti Tanzania, Upanga, Dar alisema waliwapokea vijana hao walioambatana na kamishna wa skauti kutoka Njombe aliyewaombea hifadhi kwa matarajio ya kwenda jeshini.
Mwingine aliyetapeliwa.
Akaongeza: “Jambo hilo lilitushangaza, pia tulijiuliza vijana wengi kiasi hicho wanawezaje kwenda jeshini kinyemela bila kupitia kwenye ngazi za wilaya na mikoa, tukakosa jibu huku tukiogopa wasije kuwa vijana wanaoandaliwa kwa ugaidi. Ikabidi tufanye jitihada za kumpata yule kanali na alipopatikana na kubanwa tuligundua alikuwa ni tapeli, tukamfikisha kwenye Kituo cha Polisi Salenda Bridge ili aweze kushughulikiwa.”
Kwa upande wa Dany Mwinda ambaye ni mmoja wa vijana hao anayetokea Makambako, Njombe alisema kuwa ni kweli jambo hilo liliwatokea na kuna vijana zaidi yao wako katika nyumba za kulala wageni jijini, hata hivyo, kwa kuwa suala lao lilifikishwa kwenye vyombo vya sheria imebidi wawe wapole kusubiri hatima yao.
Gazeti hili lilishuhudia vijana hao wakiwa wamezagaa kwenye ofisi za skauti wakiwa na vipara na lilifanya pia jitihada za kumtafuta kamishna wa skauti Njombe aliyewakusanya ambaye pia ndiye aliyekusanya pesa zao na kumpatia kanali feki lakini hakuweza kupatikana kupitia simu yake ya mkononi.
Baadhi ya maofisa wa polisi wa Kituo cha Salenda Bridge walithibitisha kukamatwa kwa mtu huyo, hata hivyo hawakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa wao siyo wasemaji.
Post a Comment