Mtoto wa ajabu azaliwa Dodoma
MTOTO wa ajabu amezaliwa katika kijiji cha Manchali wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma huku kichwa kikiwa kidogo na utosi ukiwa wazi.
Mama wa mtoto huyo wa kiume Joyce Elias (22) mkazi wa Kitongoji cha Mkoka kijiji cha Manchali ambako mtoto huyo alizaliwa akiwa na uzito usio wa kawaida, kilo 4 na gramu 900 na kufariki muda mfupi baadaye. Hata hivyo, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Nassoro Mzee akikanusha uvumi ulioenea kuwa mtoto huyo alizaliwa na ugonjwa wa zika.
Kutokana na hilo, Serikali imeombwa kutuma wataalamu wa afya katika kijiji hicho ili kufanya utafiti wa sababu ya kuzaliwa kwa watoto wenye matatizo ya maumbile mara kwa mara kijijini hapo.
Akizungumza na waandishi wa habari kijijini hapo jana, Diwani wa Viti Maalum, Mary Mazengo alisema kumekuwa na mfululizo wa matukio ya kuzaliwa watoto wa ajabu katika kipindi cha miezi mitatu ndani ya mwaka huu.
Alisema Januari mwaka huu alizaliwa mtoto akiwa na kichwa kikubwa huku akiwa hana jinsia ya aina yoyote ambaye alifariki dunia muda mfupi baada ya kuzaliwa. Pia Februari mwaka huu alizaliwa tena mtoto akiwa hana mikono wala kichwa huku akiwa tayari ameshakufa.
Diwani huyo alisema juzi alizaliwa mtoto mwenye kichwa kidogo huku utosi ukiwa wazi hali ambayo ilizua taharuki kwa wanakijiji kutokana na kukumbwa na hofu ya kuzaa watoto wenye matatizo.
“Serikali ilete wataalamu wa afya kijijini hapa ili kuweza kugundua ni tatizo gani limekuwa likiwakumba wakazi wa kijiji hiki,” alisema. Pamoja na hayo aliwataka kina mama kuzingatia ratiba za kliniki wakati wa ujauzito.
Alisema mara baada ya kutokea matukio hayo kijijini hapo, alianzisha kampeni za kijiji kwa kijiji ili kinamama wakajifungulie katika vituo vya afya.
Alisema lakini alijikuta akikabiliana na vikwazo kutoka kwa wanaume. Kwa upande wake, mganga wa zahanati ya kijiji hicho, Gaudensia Mpokwa alisema tukio hili ni la tatu ndani ya kipindi cha miezi mitatu la mtoto wa ajabu aliyezaliwa na Joyce Elias akiwa na uzito usio wa kawaida, kilo 4 na gramu 900, lakini kichwa kidogo kikiwa wazi sehemu ya utosini.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Mzee Nassoro alipotakiwa kuuelezea ugonjwa huo ambao unafanana na Zika kwa dalili, alisema utafiti pekee ndio unaweza kuonesha ukweli, lakini kwa haraka hizo ni dalili za kukosekana kwa baadhi ya vitamini.
“Hili ni tatizo la ukosefu wa baadhi ya vitamini ndio maana wanazaliwa hawa watoto na huu sio ugonjwa wa zika kama wengi wanavyosema kwani mpaka tufanye utafiti,” alisema.
Wakati wa mahojiano mama wa kichanga hicho, alisema kuwa kipindi chake chote cha ujauzito aliwahi kuhudhuria kliliki mara mbili tu huku akisikia maumivu sehemu za siri na alipokuwa akienda hospitali alikuwa akipatiwa dawa.
CHANZO:HABARI LEO
Post a Comment