Header Ads

LEO NI SIKU YA MOYO DUNIANI:WANANCHI KUPIMWA SHINIKIZO LA DAMU BURE.

KATIKA kuazimisha  siku ya afya ya Moyo Duniani Hospitali ya Taifa Muhimbili-MNH- leo itatoa huduma ya upimaji wa shinikizo la damu bure pamoja na kuwashauri wale watakaopatikana na tatizo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu siku ya afya ya moyo Duniani ambayo huazimishwa Septemba 29 kila mwaka , Daktari Bingwa wa magonjwa ya Moyo  Tulizo Shemu kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kitwete amesema magonjwa ya moyo yanachangia asilimia 31 ya vifo vyote vinavyosababisha takribani watu MIlioni 17. 3 kufa kila mwaka .

Inasadikika itakapofika mwaka 2030 zaidi ya watu Milioni 25 watakuwa wanapoteza maisha kutokana na maradhi hayo hasa katika nchi zilizo na uchumi wa  chini na kati.
Siku ya afya ya moyo Duniani hutoa fursa kwa watu wote Duniani kuazimisha kwa vitendo katika kujilinda na janga la magonjwa ya moyo na mishipa ya damu ambayo yanachangia vifo vingi .
Dokta  Shem  ametaja baadhi ya visababishi vinavyochangia magonjwa ya moyo kuwa ni matumizi ya tumbaku, chumvi , pombe, vyakula vyenye mafuta, kutofanya mazoezi , unene uliokithiri , kutotibu ugonjwa wa kisukari na kuwa na mafuta mengi kwenye damu.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni kuweka mazingira mazuri ya afya bora ya moyo katika sehemu zetu tunazofanyia kazi kwa kuhakikisha kila mtu anatoa mchango katika kujenga afya bora ya moyo ili kupunguza visababishi vinavyochochea magonjwa hayo.
 Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kuwa ugonjwa wa moyo husababisha vifo vya watu milioni 17.3 kila mwaka.
Ugonjwa huo ni wa pili duniani baada ya malaria unaongoza kwa kusababisha vifo vya watu.
SABABU ZA UGONJWA WA MOYO
Mienendo mibovu ya maisha ikiwamo uvutaji sigara, ulevi, ukosefu wa mazoezi ya mwili na chakula bora kwa kiasi kubwa vinachangia ongezeko la vifo vitokanavyo na ugonjwa huo nchini.
Wataalamu wa afya wanataja sababu nyingine kuwa ni umri, jinsia, historia ya familia, shinikizo la damu, kisukari, msongo wa mawazo na uchafu.
Takribani asilimia 80 ya vifo vya mapema vitokanavyo na ugonjwa wa moyo vinaweza kuzuilika kwa kuepuka sababu hizo hatarishi.
TAFITI
Utafiti uliofanyika mwaka 2012 na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na WHO, unaonyesha kuwa asilimia 26 ya Watanzania wanakabiliwa na ugonjwa wa moyo huku asilimia 20 kati yao wakiwa wanawake.
Taarifa za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa asilimia 92.6 ya Watanzania wenye ugonjwa huo hawapo kwenye matibabu licha ya kutambua kuwa wanaugua.
WHO inaeleza kuwa takriban asilimia 40 ya watu wazima katika Bara la Afrika wanaugua ugonjwa huo.

No comments