Header Ads

Waziri wa Elimu Profesa Ndalichako Aingilia kati Mgogoro wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha St. Joseph Dar es Salaam


WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako ameingilia kati mgogoro wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha St. Joseph Dar es Salaam, waliogomea kufanya mitihani na kuwataka warejee madarasani wakati matatizo yao yakishughulikiwa.

Wanafunzi hao walikuwa katika siku ya tatu ya mgomo wao jana ambapo pamoja na mambo mengine walikuwa wakilalamikia mapungufu yaliyopo chuoni hapo, ikiwa ni pamoja na maabara za kufanyia mafunzo kwa vitendo, matatizo ya kiutawala, mitaala ya kufundishia pamoja na ada.

Profesa Ndalichako aliwasili chuoni hapo jana asubuhi na kukagua mazingira ya kufundishia ya chuo hicho kwa kutembelea maabara zote chuoni hapo na kisha kwenda kuzungumza na utawala, Serikali ya wanafunzi na mwisho alihutubia wanafunzi wote.

Ndalichako baada ya kuzungumza na pande zote mbili aliagiza wanafunzi hao warejee madarasani kuendelea na mitihani yao na kuutaka uongozi wa chuo uyafanyie marekebisho mapungufu ya kiutawala yaliyojitokeza.

Aidha ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), chini ya Katibu Mtendaji wake, Profesa Yunus Mgaya kufuatilia na kuchunguza kwa makini madai ya wanafunzi hao juu ya kuwepo kwa wahadhiri wasio na sifa zinazotakiwa.

No comments