TCRA yazipiga faini E FM, Kahama FM.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandili ya TCRA, Margaret Munyagi |
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imevipa onyo na kuvipiga
faini vituo viwili vya redio kutokana na kukiuka maadili ya utangazaji.
Vituo hivyo ni Entertainment FM (E FM)
cha Dar es Salaam na Kahama FM Stereo ya Kahama, mkoani Shinyanga.
Akitoa maamuzi yaliyofikiwa na Kamati
ya Maandili ya TCRA, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Margaret Munyagi, alisema vituo
hivyo vimebainika kukiuka sheria na kanuni za utangazaji.
Amevitaka vewe na usimamizi mzuri wa
vipindi vyao.
Munyagi alisema kamati yake imekipa
onyo kali na faini ya sh milioni moja kituo cha Efm na endapo kitarudia, hatua
kali zaidi zitachukuliwa.
Alisema Januari 4 mwaka huu, kituo
hicho katika kipindi cha ‘Joto la Asubuhi’ katika kipengele cha ‘Sala ya Siku’,
kilichorushwa kati ya saa 1 hadi 3 asubuhi, Mtangazaji alihamasisha vitendo vya
wizi, ngono na uchochezi wa kidini.
Katika utetezi wake, Mkurugenzi wa
kituo hicho, Dennis Busulwa pamoja na kukiri kufanya kosa, alisema kituo chake
kilijibebesha mzigo mzito wakati bado ni wachanga katika utangazaji na kutokana
na kosa hilo waliamua kukiondoa kipengele hicho.
Kwa upande wa Kahama FM Stereo, Munyagi
alisema kituo hicho kimepewa onyo kali, kutozwa faini ya Sh 200,000 na endapo
watajirudia watapewa adhabu kali.
Januari Mosi mwaka huu, kupitia kipindi
cha ‘Wanawake’ kilichorushwa hewani kati ya saa 3 asubuhi na saa sita mchana,
mtangazaji alimhoji mwanamke aliyekuwa akifanya biashara ya kujiuza.
“Mahojiano hayo yalijikita katika
kuelezea jinsi biashara ya kujiuza inavyofanyika katika mji wa Kahama kwa
kubainisha changamoto na faida ambazo wafanyabiashara hiyo wanazipata. “Kuwepo
kwa majadiliano haya katika muda wa asubuhi kunaweza kuchochea tabia mbaya kwa
watoto kuiga vitendo vya ufanyaji ngono,” alisema.
Katika utetezi wake, Meneja wa Kahama FM
Stereo, Marco Mipawa, alikiri kikiuka sheria na kanuni za utangazaji na kuahidi
kwamba tatizo hilo halitajirudia tena.
Post a Comment