Siku 67 za Ombeni Sefue Ikulu Kabla ya Kutumbuliwa JIPU Jana
JANA ilikuwa siku ambayo Rais John Magufuli alitoa uamuzi mzito wa kubadilisha nafasi za uongozi wa ngazi ya juu zaidi kwa viongozi ambao amefanya nao kazi baada ya kumuondoa Balozi Ombeni Sefue aliyekuwa katibu Mkuu Kiongozi, akiwa mstari wa mbele kutangaza wanaotumbuliwa majipu.
Balozi Ombeni Sefue alikuwa kivutio cha wengi kwenye vyombo vyahabari kutokana na kutoa taarifa za kutenguliwa uteuzi kwa watumishi waandamizi wa umma, lakini jana hali ilikuwa tofauti baada ya kibao kugeuka.
Ombeni Sefue aliibukia kuwa kipenzi cha vyombo vya habari katika muda mfupi aliofanya kazi na Rais Magufuli, huku mitaani akivuta wengi karibu na runinga kila alipoonekana, hasa kutokana na wananchi kutarajia kusikia habari za kutumbuliwa kwa majipu ambao umekuwa ukifanywa na Serikali tangu Rais aapishwe Novemba 5, 2015.
Alianza kuchukuliwa na wengi kuwa ni mchapakazi na muadilifu na angeweza kwenda na kasi ya Rais Magufuli, ambaye amekuwa akihimiza mambo hayo na kusisitiza kuwa mtu asiyeweza kwenda na kasi yake, hatamvumilia.
Hakuna aliyekuwa na shaka na Balozi Sefue. Hata gazeti la Diralilipotoa habari mfululizo kwenye matoleo mawili likimuhusisha na ushauri mbaya kwa Rais na pia utafutaji wa mjenzi wa daraja la Kigamboni, wengi hawakuweza kuamini, hasa kutokana na kuonekana kuwa karibu na Rais.
Lakini uamuzi wa Rais kumteua Balozi Kijazi kushika nafasi yake, unaweza kuibua mjadala mpya kuhusu ujenzi wa daraja hilo na mabadiliko yanayofanywa na Rais.
Uteuzi wa Katibu Mkuu Kiongozi mpya umekuja siku 67 tangu Rais Magufuli atangaze kuteua makatibu wakuu 29 wapya Desemba 30, 2015 huku Sefue akihakikishiwa kuendelea kukaa Ikulu kwa mwaka mmoja zaidi.
Uteuzi huo pia umekuja siku chache baada ya gazeti la Dira kuanza kuandika jinsi Ikulu ilivyoshauriwa vibaya kuhusu uteuzi wa mkurugenzi mkuu wa Bohari ya Madawa (MSD), ingawa Idara ya Habari (Maelezo) ilitoa tamko kali la kukanusha na kulitaka gazeti hilo liombe radhi, kitu ambacho hakijafanyika.
Uteuzi huo pia umekuja wakati kukiwa na sarakasi ya uteuzi wa Carina Wangwe kuwa kaimu mkurugenzi mkuu wa NSSF na uamuzi huo kutenguliwa saa tano baadaye (kutangazwa saa 11:150 jioni na kutenguliwa saa 4:15 usiku).
Katika sakata hilo, Sefue hakutangaza uteuzi huo ila alisema kuwa mamlaka ya kuteua ni ya Rais lakini ya kukaimu kuna taratibu zake, ambazo hakuzitaja. Alisema Wangwe alitakiwa kuwa mwangalizi.
Pia Balozi Kijazi, ambaye anamrithi Sefue kwenye nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi, ndiye aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu wakati pendekezo la ujenzi wa daraja la Kigamboni lilipotolewa na baadaye kupitishwa huku likikumbana na upinzani mkalitoka kwa Kijazi na Magufuli ambaye wakati huo alikuwa ni Waziri wa JK.
Balozi Kijazi aliondolewa wizara hiyo na kupelekwa ubalozini nchini India mwaka 2007 huku Magufuli akihamishiwa Wizara ya Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo mwaka 2008.
Balozi Sefue alizaliwa Agosti 26, 1954 wilayani Same, Kilimanjaro. Alisomea Utawala na Sera za Umma kwenye Chuo cha Uongozi cha Mzumbe, ambacho sasa kinaitwa Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Baadaye alipata shahada ya uzamili katika fani hiyo kwenye Chuo Kikuu cha Masomo ya Kijamii cha The Hague nchini Uholanzi mwaka 1981.
Pia ana astashahada ya uzamili ya masuala ya uhusiano wa kimataifa aliyoipata Chuo cha Diplomasia kilichopo Dar es Salaam.
Pia ana cheti cha usuluhishi wa kimataifa, matatizo ya kiuchumi na kijamii ya nchi zinazoendelea. Balozi Sefue na mkewe Anita wana watoto wawili, wa kiume na kike.
Amekuwa balozi wa Tanzania Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2007. Kabla ya hapo, alikuwa balozi wa Tanzania nchini Canada (2005-07).
Balozi Sefue aliachana na kazi ya udiplomasia mwaka 1993 na kwenda kufanya kazi ya kuandika hotuba za rais na pia kuwa msaidizi binafsi wa Rais Ali Hassan Mwinyi. Baada ya uchaguzi wa mwaka 1995, Rais Benjamin Mkapa aliendelea naye hadi mwaka 2005 wakati alipoachia ngazi.
Balozi Sefue alifanya kazi kwa karibu na Mkapa wakati akiwa Kamisheni ya Afrika (maarufu kama kamisheni ya Blair) ambayo ilitengeneza ripoti iliyojulikana kwa jina la “Our Common Interest: Report of the Commission for Africa in March 2005”, na kushiriki naye kwenye kikao cha marais wa nchi nane tajiri duniani (G8) ambacho kilijadili ripoti hiyo.
Pia alifanya kazi kwa karibu na Mkapa wakati akiwa mwenyekiti mwenza wa kamati iliyochambua athari za utandawazi kijamii ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) kati ya mwaka 2002-2004.
Rais Kikwete alimteua kuwa Katibu Mkuu Kiongozi Desemba 31, 2011 na amedumu na wadhifa huo mpaka jana, huku akifanya kazi na Rais wa Awamu ya Tano, Dk Magufuli kwa siku 67 tu licha ya kuwa aliongezewa mwaka moja.
Post a Comment