Header Ads

Ziara ya Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa Yawapa Kiwewe Wakuu wa Wilaya Kagera


Kasi ya kutumbua majipu imeonekana kuwatia kiwewe wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Kagera kwa kufanya kazi na mikutano ili kuhakikisha hakuna makosa yatakayoonekana wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa ya kukagua miradi ya maendeleo inayoanza kesho kutwa.

Kwa wiki moja sasa, wakuu hao wanafanya mikutano ya kila siku na kukagua miradi hiyo ili kuhakikisha hakuna makosa yanayoweza kusababisha kutumbuliwa majipu.

Mkuu wa Wilaya ya Missenye, Festo Kiswaga alisema mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa wamechukua tahadhari kwa kuhakikisha kila eneo liko salama.

“Tunafanya maandalizi kila sehemu na idara maana ni vigumu kutabiri Waziri Mkuu atatembelea wapi,” alisema Kiswaga.

Alisema ratiba ya maeneo atakayotembelea Waziri Mkuu imebadilika mara tatu tangu walipotaarifiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Jackson Msome alisema wanalazimika kuzingatia kanuni ya mchezo wa soka kwa kuelekeza maandalizi kila idara kuanzia sehemu ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji.

“Ni lazima kujiandaa kila idara kufanikisha ziara ya Waziri Mkuu kwa sababu hatuwezi kujiamini na ratiba bila kuchukua tahadhari ya ziara za kushtukiza eneo lolote,” alisema Msome.

Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, Darry Rwegasira alisema licha ya ratiba kuonyesha kuwa Waziri Mkuu atatembelea na kuzindua jengo la upasuaji katika kituo cha Afya cha Nyakanazi, wamefanya maandalizi katika eneo lote ili kuepuka kushtukizwa iwapo ratiba itabadilika ghafla.

Mfanyabiashara mjini Bukoba, Dennis Gregory alisema wanakusudia kuwasilisha kwa Waziri Mkuu changamoto ya bei ndogo ya kahawa inayouzwa nchini ikilinganishwa na Uganda.

No comments