Header Ads

Mbunge wa CCM Faustine Ndugalile Awakosoa Mawaziri wa Rais Magufuli


Mbunge  wa Kigamboni, Dar es Salaam ,Faustine Ndugalile (CCM) amekosoa utendaji wa mawaziri wa serikali ya Rais Magufuli  akisema wanatishia wafanyakazi badala ya kuwaelekeza katika utendaji wao.

Katika ujumbe aliouweka kwenye mtandao wa twitter kwa lugha ya kiingereza, Ndugalile ameandika: "Ministers should encourage or provide practical solutions to problems instead of barking orders and terrorizing civil servants."

 Kwa lugha ya kiswahili, mbunge huyo alimaanisha:" Mawaziri wanatakiwa kuwatia moyo au kutoa suluhisho kwa matatizo badala ya kufoka na kuwatisha watumishi wa umma."

Alipoulizwa kuhusu ujumbe huo,Ndugalile alikiri kuwa ni wake na kusisitiza kuwa ni wajibu wake kama mbunge kuisimamia serikali.

"Mimi ni mbunge, kazi  ya  mbunge ni kuisimamia serikali.Ikifanya vizuri tutaisifia, ikikosea tutaikosoa.

"Nimesema baadhi  ya  mawaziri- sio wote wanawatisha wafanyakazi. Kazi ya kiongozi ni kuonyesha uongozi na si kuwa bosi.

"Inaonyesha kuna baadhi ya  mawaziri wamekuwa kila kitu ;wao ndo mawaziri,ndo wakurugenzi, ndo wakuu wa idara..." alisema

Ndugalile anakuwa mbunge wa kwanza wa CCM kukosoa kasi ya mawaziri wa Rais Magufuli, huku mwenyekiti wa chadema Freeman Mbowe akimkosoa Rais Magufuli kwa kuwasimamisha baadhi ya watendaji wa serikali bila kufuata taratibu za utumishi wa umma na sheria za kazi.

Akifafanua zaidi, Ndugalile alisema baadhi ya mawaziri wamekuwa wakitoa amri zisizotekelezeka na zinazotofautiana  na  ilani ya uchaguzi ya CCM  ya mwaka 2015.

"Kuna baadhi ya mawaziri wanatoa amri zisizotekelezeka.Kwa mfano, mtu anatoa amri itekelezwe ndani ya siku 3, itawezekanaje? umewapa rasilimali za kutekeleza?" alihoji Ndugalile.

Hata hivyo, Ndugalile alisema anaunga mkono hatua za kudumisha nidhamu kwa watumishi wa umma zinazofanywa na mawaziri.

No comments