Kubenea Akana Kumtukana Paul Makonda....Kesi Yaahirishwa Hadi March 10.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu hakutoa lugha chafu dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda kama inavyodaiwa.
Kubenea alitoa kauli hiyo jana wakati akitoa utetezi huku akiongozwa na wakili wake, Peter Kibatala mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
“Mimi sijasema hayo maneno kuwa Makonda ni mjinga, mpumbavu, kibaka na cheo chenyewe cha kupewa, bali nilimwambia wewe umeteuliwa na Rais na mimi nimechaguliwa na wananchi,” alidai.
Kubenea aliendelea kudai kuwa Desemba 14, 2015, katika kiwanda cha Tooku Garments Co. Ltd kilichopo Mabibo External kwenye mgomo wa wafanyakazi wa kiwanda hicho, alimwambia Makonda hawezi kufunga mkutano bila ya yeye kuzungumza kwa sababu ni mwakilishi wa wananchi.
Alidai kuwa Makonda alimjibu kila alipokuwa akizungumza kuwa yeye ndiye mtu wa mwisho kwa kuwa ni rais wa Kinondoni.
“Nilimjibu na mimi ni mbunge, nimeteuliwa na wananchi, lazima aheshimu uwapo wangu pale,” alidai.
Kubenea alidai kutokana na msimamo wa Makonda wa kutotaka kumpa nafasi ya kuzungumza na wafanyakazi, alimwambia hajavamia mkutano huo bali aliitwa.
“Nikamwambia mimi siyo kibaka bali nimechaguliwa na watu, baada ya kauli hiyo, alimuamuru Mkuu wa Upelelezi wa Kituo cha Polisi Magomeni, Denis anikamate nikapumzishwe mahabusu,” alidai.
Alidai kuwa mkuu huyo wa wilaya, aliamuru pia kukamatwa kwa raia mmoja wa China anayedaiwa kuwanyanyasa wafanyakazi hao ili achunguzwe.
Kesi hiyo itaendelea Machi 10, mwaka huu. Kubenea anadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 14, 2015 katika Kiwanda hicho.
Post a Comment