Header Ads

Nape Nnauye Ataka Magazeti Ya Serikali Yamsaidie Rais Magufuli Kutumbua Majipu Kwa Kuibua Uozo Serikalini


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametaka magazeti ya Serikali kumsaidia Rais John Magufuli, kutumbua majipu kwa kuibua uozo serikalini.

Akizungumza katika kikao cha wafanyakazi wa Kampuni ya Tanzania Standard (Newspapers) Ltd Dar es Salaam jana, inayochapisha magazeti ya Daily News, HabariLeo na Spotileo, Nape ametaka magazeti hayo yasimung’unye maneno kwa kuandika ukweli; kwenye nyeusi yaandike nyeusi na kwenye nyeupe, yaandike nyeupe.

Alisema vyombo vya habari vya Serikali vina wajibu wa kumsaidia Rais kutumbua majipu kwa kuandika habari bila woga, upendeleo wala kuomuonea mtu, ili kama kuna dosari ziko mahali ziibuliwe kwa lengo la kupata suluhu.

“Unajua vyombo vya habari vinaaminika na vinasomwa na wengi na hasa wananchi wanapotaka ukweli wa jambo, wanaangalia kama limeandikwa, sasa kama jambo litaandikwa kwa kufichwa fichwa haitaisaidia Serikali, kama ni nyeusi sema nyeusi, kama ni nyeupe sema nyeupe na hiyo ndiyo suluhu,” alisisitiza Nape.

Alisema majipu yanayoendelea kutumbuliwa na Rais, mengine yanaibuliwa na vyombo vya habari na ili kumsaidia na kusaidia Taifa, vyombo vya habari vya Serikali lazima viibue hayo, pia viaminiwe mpaka na watumishi wa Serikali, wavitumie kuibua uozo.

Nape alisisitiza kwamba kuficha ukweli kwenye jambo ovu, ni kuendelea kuharibu hivyo kuibuliwa kwa maovu kutaisaidia Serikali na watendaji wake kuchukua hatua madhubuti.

 “Kuna hili jambo la baadhi ya watendaji kusema mfumo hautaki hili, hakuna cha mfumo ni maneno yao wanayatumia kama kichaka cha kufanya uchafu,” alisema Nape.

Nape alitoa onyo kwa watendaji wa serikali kuacha tabia ya kuzuia habari zisitoke kwa maslahi yao na kutaka wenye pingamizi ya kutoka kwa habari, wawasiliane naye na si kuingilia chombo cha habari.

No comments