Header Ads

ILI KUSIMAMIA MATUMIZI MAZURI YA PESA YAKO KATIKA BIASHARA FANYA YAFUATAYO.

Kwenye ujasiriamali na hata biashara kwa ujumla fedha ndio damu au uhai wa biashara yako. Pamoja na kuwa na mpango mzuri, na hata ubunifu kwenye ujasiriamali bado utahitaji fedha kwa ajili ya kuzalisha au kununua bidhaa ili uweze kuuza. Na hata baada ya kuzalisha au kununua, mapato unayopata ni muhimu sana kusimamiwa vizuri kama unataka kuendelea kuwepo kwenye biashara.

Leo utapata nafasi ya kujifunza misingi mitano ya usimamizi wa fedha kwenye biashara. Misingi hiyo ni;

1. Tenga matumizi ya biashara na matumizi yako binafsi.
Moja ya kosa kubwa linalofanywa na wajasiriamali wengi ni kuchanganya matumizi binafsi na matumizi ya biashara. Ni vigumu sana kuona faida na ukuaji wa biashara kama fedha ya matumizi yako binafsi inatoka moja kwa moja kwenye fedha ya biashara. Utaona unauza sana lakini fedha huzioni. Ili uweze kuona ukuaji halisi wa biashara na ujasiriamali tenga fedha za biashara na fedha za matumizi binafsi.

2. Jilipe mshahara kutoka kwenye biashara yako.
Najua unajiuliza sasa nitaishije kama siwezi kuchanganya matumizi ya biashara na matumizi binafsi wakati biashara ndio shughuli inayoniingizia kipato cha kuendesha maisha. Ili uweze kuwa na mtengano mzuri kati ya fedha ya matumizi binafsi na matumizi ya biashara jilipe mshahara. Unaweza kuamua kujilipa mshahara kwa siku, wiki, au mwezi. Baada ya kujilipa mshahara wako usiguse tena fedha ya biashara, hili linahitaji nidhamu ya kutosha. Njia nzuri ya kujipangia mshahara ni kujilipa kamisheni, yaani unajilipa asilimia fulani ya faida unayopata kwenye biashara. Utakapohitaji kupata mshahara mkubwa zaidi utasukumwa kufanya biashara zaidi ili upate faida kubwa na baadae kamisheni kubwa.

3. Jua tofauti ya mauzo na faida.
Hiki ni kitu rahisi sana kwenye ujasiriamali ila bado wengi wanashindwa kukifuata. Mauzo ni tofauti kabisa na faida. Kwa mfano umenunua mfuko wa sukari kwa tsh elfu 40 na kuuza tsh elfu 60 umepata faida ya tsh elfu 20 si ndio? Sasa weka fedha ya kufikisha mfuko huo kwenye eneo la biashara, weka muda uliotumia kuuza mfuko huo, weka kodi ya eneo la biashara. Ukijumlisha vyote hivi unaweza kujikuta unabaki bila ya faida yoyote. Nachotaka ujifunze kwenye mfano huu ni kwamba unaweza kuona unauza fedha nyingi sana ila hupati faida kwa sababu hujapiga vizuri mahesabu yako.

4. Epuka gharama zisizo za msingi
Sio kila kitu unachoona wajasiriamali wenzako wanafanya na wewe inabidi ufanye, hasa pale kitu hicho kinapokuwa ni gharama kwenye biashara yako. Tumia fedha kwenye matumizi ya msingi na baadae utaendelea kukua kidogo kidogo. Kama ndio unafungua ofisi yako mpya kuna vitu vingi unaweza kuepuka gharama kwa kufanya manunuzi yako vizuri. Vitu kama thamani, unaweza kununua zinazokidhi mahitaji yako na kwa bei ambayo ni nzuri kwako.

5. Fanya mahesabu ya mara kwa mara kwenye biashara yako.
Hili ni tatizo la msingi na ndipo wajasiriamali wengi wanashindwa. Watu ni wavivu wa kukaa chini na kufanya mahesabu ya biashara zao. Wengine wanaamini kwa vile biashara wanasimamia wenyewe basi wanajua kila kitu hivyo hakuna haja ya kupiga hesabu moja moja kwa kila bidhaa aliyonunua na kuuza. Hata uwe makini kiasi gani ni lazima kuna sehemu utakosea au kupitiwa. Unapofanya mahesabu mara kwa mara kwenye biashara yako inakusaidia kujua ni wapi fedha zinapotelea na kudhibiti mianya hiyo. Pia inakujuza ni vitu gani vyenye faida kubwa na vipi ambavyo vina faida ndogo.

Mafanikio kwenye ujasiriamali yanahitaji kujipanga na kujua ni kitu gani unafanya. Ni muhimu sana kuwa na usimamizi mzuri wa fedha ili uweze kufanikiwa kwenye ujasiriamali.

No comments