Amchoma mtoto kwa kutoanika shuka alizokojolea.
LICHA ya Serikali kukemea vitendo vya kikatili dhidi ya watoto wadogo, mama mmoja wilayani Igunga mkoani Tabora, Kulwa Shasumuni amemchoma moto mwanawe Hassani Faustino (9) kwenye mkono wa kushoto kwa kile alichodai ameshindwa kuanika shuka zake alizokojolea kitandani.
Wakizungumza kwa machungu kwa nyakati tofauti, baadhi ya majirani ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini, walidai mama huyo amekuwa akimfanyia vitendo vya kikatili mwanawe mara nyingi hata wanapomzuia amekuwa akiwafokea na kuwaambia huyo si mtoto wao.
Aidha, majirani hao walidai walisikia kelele za mtoto Hassani “mama nakufa” na walipochungulia dirishani kwenye nyumba hiyo, walimwona mama huyo akiwa amemweka mtoto wake kwenye moto wa kuni na ndipo wao walilazimika kupiga kelele na hatimaye alimwachia.
Hata hivyo, majirani hao walibainisha kuwa mama huyo aliamua kumpeleka mtoto hospitali ya wilaya ambapo alilazwa wodi namba 8 kwa ajili ya matibabu kutokana na moto aliochomwa mkono wa kushoto.
Baada ya wiki mbili, mama huyo aliomba ruhusa hospitali ya kurudi nyumbani akidai atakuwa akimpeleka kusafisha kidonda jambo ambalo hakulitekeleza, badala yake alimfungia ndani kwa zaidi ya mwezi mpaka wananchi walipogundua na kutoa taarifa Ustawi wa Jamii waliofika kumchukua mtoto na kumrudisha hospitali.
Akizungumza akiwa katika Wodi Namba 8 katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga, Hassani alisema alikojoa kitandani kwa bahati mbaya na mama yake alipogundua, alimwamuru azianike shuka alizokojolea jambo alilosahau kufanya, ndipo mama yake alimkamata na kumtupia katika moto wa kuni uliokuwa ukiwaka kwa kasi.
Mama huyo alikiri kufanya ukatili huo akidai hasira zilikuwa zimemshika hivyo hakujua kama majivu hayo yana moto, huku Diwani wa Kata ya Igunga, Charles Bomani akilaani ukatili huo na kuitaka Serikali ya Wilaya kuokoa maisha ya mtoto huyo huku akishangazwa na ukimya wa Polisi kutomkamata mama huyo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Igunga, Abdallah Ombeni alisema hali ya mtoto huyo ni mbaya na wanajitahidi kuhakikisha wanamnusuru.
Post a Comment