Header Ads

Aliyekuwa na Mtikila siku ya kifo afikishwa polisi!

 Mchungaji Christophar Mtikila enzi za uhai wake.

Mchungaji Patrick Mgaya (pichani) ambaye alikuwa na Mchungaji Christophar Mtikila siku anapatwa na mauti kutokana na ajali ya gari mkoani Pwani wakitokea Njombe kuelekea jijini Dar, amefikishwa katika Kituo cha Polisi, Njombe, Uwazi limenasa.

Kwa mjibu wa mke wa marehemu Mtikila, Georgia, Mchungaji Mgaya amefikishwa polisi na watu wengine kwa madai kuwa wamezuia vyombo vya muziki vilivyokuwa vikitumika katika kampeni za siasa za Democratic Party (DP) ambavyo walikuwa wameviazima kutoka kanisani kwao marehemu.
Mama Georgia alisema kwamba walifungua mashtaka polisi Novemba 3, mwaka huu na shauri hilo likapewa jalada namba NJ/RB/3009/2015 katika Kituo cha Polisi Njombe na tayari Mchungaji Mgaya na wenzake wameshahojiwa kuhusiana na sakata hilo.

 Mchungaji Patrick Mgaya.

“Mchungaji Mgaya ndiye aliyepewa hivyo vyombo na marehemu Mtikila kupeleka Njombe kwa ajili ya kampeni kipindi hicho kabla ya uchaguzi na ni vya Kanisa la Full Salvation ambalo Mchungaji Mtikila alikuwa kiongozi wake mkuu, akaamua kuazimisha kwa chama kwa ajili ya kufanyia kampeni.

“Nashangaa kwa sasa Mgaya anasema kwamba vyombo ni vyake na kuwa yeye ndiye aliyevinunua hivyo hawezi akavikabidhi kwa mtu yeyote kitu ambacho si kweli, najua haki itatendeka, nawategemea polisi kufanya uchunguzi wa kina na kila kitu kitajulikana,” alisema mama huyo huku machozi yakimbubujika.

Mchungaji Mgaya alipoulizwa juu ya sakata hilo kwa njia ya simu juzi Jumapili alikiri kufahamu suala hilo na akasema suala hilo amemuachia Mungu.

“Mimi kwa sasa siko tayari kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu suala hilo nimemuachia Mungu.

“Tena basi suala hilo nimeshalimaliza polisi Njombe sasa sipendi kabisa kulizungumzia tena,” alisema Mchungaji Mgaya.

No comments