Header Ads

Rais Kikwete Awaonya Wanaopanga Kulinda Kura Vituoni.

RAIS Jakaya Kikwete, jana ametumia kumbukumbu ya miaka 16 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akiwataka Watanzania kuchagua viongozi katika uchaguzi wa mwaka huu watakaodumisha amani.
 
Alitumia kumbukumbu hiyo kuwapiga vijembe baadhi ya wanasiasa wanaotaka kuchaguliwa kwa kutumia rushwa, misingi ya udini na ukabila ndani ya vyama vyao.
 
Akihutubia wakati wa kumbukumbu hiyo iliyoenda sambamba na Kilele cha Mbio za Mwenge katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma jana, Rais Kikwete, alisema taifa halipo tayari kuwapisha viongozi ambao wanabeba udini na ukabila katika chama chao.
 
Alisema Watanzania wanapaswa kuchagua kiongozi ambaye ataweza kuwaletea mabadiliko na si yule anayekumbatia rushwa,udini na ukabila.
 
Alisema endapo kiongozi huyo ataweza kupata fursa ya kuongoza nchi ataweza kuweka watu wa kabila moja au dhehebu lake katika utawala wake.

Rais Kikwete alisema wapo wagombea ambao wanasaka uongozi kwakutaka wachaguliwe kwa misingi ya madhehebu yao ili kuongoza nchi. 
  
"Kufanya hivyo ni kuleta hatari, hivyo Watanzania wasikubali kugawa uongozi kwa udini," alisema.

Akizungumzia rushwa, Dkt. Kikwete alisema wapo viongozi ambao waliweza kuongoza ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na sasa wametoka ndani ya Chama hicho na kwenda katika Chama kingine huku wakipewa heshima za kugombea nafasi za juu za uongozi, lakini hata siku moja hawajawahi kuzungumzia suala la rushwa wakati rushwa ni tatizo kubwa kwa taifa.

Alisema ni dhahiri viongozi kama hao wanaonekana wao ni miongoni mwa viongozi wanaokumbatia rushwa bila kujali masilahi ya Watanzania.

Rais Kikwete alisema viongozi wanapaswa kutokuwa na vigugumizi wakati kuongelea suala la rushwa. "Wanapaswa kuikemea kwa pamoja kwani rushwa ni adui mkubwa wa haki hivyo si suala la kuchekea na kufumbia macho kama wafanyavyo baadhi ya viongozi," alisema.

Rais Kikwete alisema hivi karibuni baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wamewaambia wafuasi wao kutoondoka katika vituo vya kupigia kura kwa lengo la kulinda kura.
  
Alionya kwamba kufanya hivyo kunaweza kuleta vurugu zisizo za lazima.

"NEC na ZEC imeshatoa angalizo la kutofanya hivyo siku ya kupiga kura kwani ni kinyume cha sheria huku Tume tayari imeeleza kuwa ndani ya vyumba vya kupigia kura kutakuwa na mawakala hivyo hakuna sababu ya wafuasi kusimama nje wala kusogelea kituo cha kupiga kura," alisema Kikwete.

Alisema wafuasi wasiwe tayari kuchuuzwa na viongozi wao wa siasa kwani kufanya hivyo ni uvunjifu wa Sheria utakaosababisha kuhamasisha uvunjifu wa sheria.

"Nawahakikishia Watanzania kuwa njama zao, ovu na nia zao zinajulikana na kamwe Serikali haitafumbia macho na wala njama hizo kufanikiwa tumejipanga endapo watu watakiuka agizo la NEC na ZEC sheria itafuata mkondo bila kumwonea haya mtu yeyote yule," alisema

No comments