Header Ads

MAGUFULI AWASHUKIA TANESCO KUKATIKA KWA UMEME ASEMA WAJIANDAE.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, Dk Magufuli alisema kama watendaji wa shirika hilo wanamuhujumu kwa kumzimia umeme, wajiandae kutoka kwenye viti vyao akiingia ofisini kwani bado siku 18 tu za kuingia Ikulu.

Dk Magufuli, ambaye amekuwa akisisitiza kwenye mikutano yake kuwa hatavumilia watendaji wazembe, alisema mawaziri wa Wizara ya Nishati na Madini na watendaji wajiandae kuachia nafasi zao kwani hataweza kuwavumilia.

Alisema tatizo la umeme, ambalo linaonekana kuwa sugu, limekosa majibu ya uhakika.

“Ninajua mawaziri wapo kwenye kampeni, lakini nao wajiandae zimebaki siku 18 tu,” alisema Dk Magufuli.

Awali Tanesco ilisema kuwa tatizo la sasa la umeme lingedumu kwa wiki moja kwa kuwa ilikuwa ikishughulikia kuunganisha mitambo ya kufulia umeme na mabomba ya gesi asilia, lakini mapema wiki hii imeeleza kuwa kazi hiyo inaweza kuchukua muda mrefu zaidi kutokana na gesi hiyo kuwa na uchafu uliotokana na uwekaji mabomba, msukumo kuwa mdogo na kusubiri matokeo ya vipimo vilivyopelekwa nje ya nchi.

Hali kadhalika, uwezekano wa kutumia umeme unaofuliwa kwa kutumia maji, haupo kwa sasa kutokana na mabwawa kukauka.

Awali, katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema ni jambo ambalo haliwezekani kwa tatizo la umeme kushindwa kupatiwa ufumbuzi kwa muda mrefu.

“Hatutaki majibu mapesi kwenye maswali magumu,” alisema Kinana.“Kama wanabadilisha mitambo sasa kutumia gesi, kwanini hawakujiandaa?”

Kinana alisema viongozi ambao wamekuwa wakitoa majibu kuhusu sakata la umeme ni wale ambao wanaishi nyumba zenye mashine za jenereta, hivyo hawajui adha za wananchi.

“Kuna wananchi kazi zao ni vinyozi, sasa wanapokosa umeme ujue unawaathiri sana,” alisema.

Katika mkutano huo, mamia ya wananchi walipaza sauti kulalamikia tatizo la umeme wakisema kuwa ni kero na hivyo kumfanya Kinana, ambaye amekuwa akilaumu watendaji wa Serikali, azungumzie tatizo hilo. Tazama Video Hii 

No comments