Header Ads

Lowassa Kuhudhuria Mazishi ya Mtikila.


MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chadema kupitia mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa, anatarajia kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrati (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, imefahamika.

Duru za siasa kutoka ndani ya Ukawa, zimebainisha kwamba, licha ya kusambazwa kwenye mitandao kwa taarifa za Mchungaji Mtikila kumshambulia Lowassa kwa maneno kabla ya kifo chake, lakini mgombea huyo wa Ukawa amepanga kwenda kuhudhuria mazishi hayo kutokana na sababu kadhaa.

“Kwanza amesema Mtikila ni miongoni mwa waasisi wa siasa za mageuzi nchini na ametoa mchango mkubwa katika mambo mbalimbali yaliyobadilisha demokrasia na kupanua wigo wa siasa za upinzani,”kilisema chanzo  kutoka ndani ya Ukawa.

Lakini pili, kwa mujibu wa chanzo hicho, ni kushindwa kuhudhuria misiba kadhaa ya wanasiasa waliofariki dunia katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

“Hakuhudhuria msiba wa Peter Kisumo kutokana na kususa baada ya msafara wake kuzuiliwa, lakini hakwenda kumzika mgombea wa Chadema katika Jimbo la Lushoto, Mohammed Mtoi na hakuhudhuria msiba wa aliyekuwa Waziri wa Utumishi, Celina Kombani, ambaye alikuwa anatetea kiti chake katika Jimbo la Ulanga Mashariki kupitia CCM,” kilibainisha chanzo hicho.

Mchungaji Mtikila alifariki kwa ajali ya gari Jumapili, Oktoba 4, 2015 katika Kijiji cha Msolwa mkoani Pwani wakati akirejea Dar es Salaam kutoka Njombe alikokwenda kufanya mkutano wa hadhara. 
  
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi ya mwanasiasa huyo, David Mwaijojele, mwili wa marehemu utasafirishwa leo kwenda Ludewa, Njombe na endapo kila kitu kitakwenda sawa, Mchungaji Mtikila atapumzishwa kaburini kesho.

No comments