WanaCCM wavamia ofisi wakihoji kuenguliwa Aeshi.
WAKAZI na wapigakura wa Jimbo la Sumbawanga Mjini mkoani Rukwa wamevamia Ofisi ya CCM wilaya ya Sumbawanga Mjini, wakidai kupewa maelezo ya kina kuhusu kuenguliwa jina la mbunge aliyemaliza muda wake, Aeshi Hilaly.
Kwa mujibu wa mashuhuda, mashabiki wa mwanasiasa huyo ambaye aliibuka kidedea katika kura za maoni kwa kujizolea kura 13,661, walivamia na kusababisha vurugu katika ofisi hiyo ya chama wakipinga kuenguliwa kwa jina Hilaly na Kamati ya Siasa ya Wilaya.
Hata hivyo, wakati mashabiki hao wakiwa wamevamia ofisi hizo za CCM , Kamati ya Siasa ya Mkoa ilikuwa inaendelea na vikao vyake vya kupendekeza wagombea wa kura za maoni katika majimbo ya mkoani huo.
Kutokana na vurugu hizo, Hilaly alilazimika kufika katika ofisi hizo na kuwatuliza mashabiki wake hao, akiwaeleza kuwa kikao cha kamati ya siasa ya mkoa kinaendelea.
Alisikika akiwa katika ajengo ya ofisi hizo, akilalamika kuwa mkusanyiko huo unaweza kumharibia zaidi.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kumekuwepo na kuvuja kwa siri za kikao cha kamati ya siasa ya wilaya ya Sumbawanga Mjini, kuwa mgombea huyo amewekea alama mbaya pamoja na mgombea mwenzake, Anyosisye Kiluswa ambaye aliibuka wa pili katika kura za maoni kwa kupata kura 1056.
Wagombea wengine katika kura hizo za maoni ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mbulu, Fortunatus Fwema aliyepata kura (727) , Frank Mwalembe (524) , Mathias Koni (292), Victor Sanga (83) , Gilbert Simya (58) na Sospeter Kansapa (38) . Wengine ni Paschal Senga (25), Mbonimpae Mkolowoko (22).
Wakati vurugu hizo zikitokea wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa walikuwa wanakutana katika ofisi za CCM mkoa wa Rukwa.HABARI LEO.
Post a Comment