Header Ads

LOWASSA KUCHUKUA FOMU ZA URAIS NEC KESHO.

MGOMBEA urais wa vyama vinne vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kesho atachukua fomu ya uteuzi wa urais katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Akizungumzia katika Makao Makuu ya chama cha NCCR-Mageuzi Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu, alisema msafara wa kumsindikiza Lowassa, utaanzia Makao Makuu ya CUF, Buguruni asubuhi saa tatu kwenda NEC ambapo saa tano asubuhi mgombea huyo atachukua fomu.
Baada ya kuchukua fomu, Lowassa ambaye alijiuzulu uwaziri mkuu kwa kashfa ya kuingiza Serikali katika mkataba wa kufua umeme wa kampuni feki ya Richmond na baadaye kuchujwa katika kinyang’anyiro cha kuwania urais kupitia CCM, atakwenda Makao Makuu ya Chadema, Kinondoni.
“Tumemaliza vikao vya ndani sasa tunatoka nje, na Jumatatu (kesho), mgombea wetu Lowassa akiwa na mgombea mweza, Juma Haji Duni watachukua fomu NEC. Msafara utaanzia CUF, kuonesha umoja wetu,” alisema Mwalimu.
Alisema baada ya hapo kazi ya kuzunguka mikoani kutafuta wadhamini itaanza Agosti 14, baada ya mgombea huyo kuhudhuria maziko ya Muasisi wa TANU na CCM, Marehemu Peter Kisumo yanayotarajiwa kufanywa Agosti 13, mkoani Kilimanjaro.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha NLD, Tozzy Matwanga, aliwaomba Watanzania na wafuasi wa Ukawa kujitokeza kumsindikiza Lowassa kuchukua fumo kwani kufanya hivyo ni kuunganisha nguvu ya ushindi.

Akizungumzia ugawaji majimbo, Mwalimu alisema kazi imekamilika na wakati wowote kuanzia leo watatangaza mgawanyo wa hayo majimbo.HABARI LEO

No comments