Header Ads

ULINZI WAIMARISHWA KWA MAGUFULI.



 Saa chache baada ya Dk John Magufuli kutangazwa kuwa mteule wa CCM kuwania urais, ulinzi umeimarishwa kwa mgombea mwenyewe, nyumbani kwake eneo la Ada Estate, Dar es Salaam na jimboni Chato mkoani Geita.
Muda mfupi baada ya kuwapo taarifa kuwa Magufuli anaongoza kura za wajumbe wa Mkutano Mkuu, aliongezewa ulinzi usiku huo na hadi jana muda wote, alionekana akiwa na walinzi watano.
Jimboni Chato, nyumbani kwake eneo la Rubambambangwe, polisi walionekana wakitanda tangu jana asubuhi tofauti na siku nyingine.
Askari hao wakiongozwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Chato, Alex Mkama walionekana nyumbani hapo tangu asubuhi hata kabla matokeo yaliyompa ushindi Dk Magufuli  hayajatangazwa.
Mwandishi wa habari hizi ambaye alikwenda nyumbani kwa Dk Magufuli kuzungumza familia yake, hakuruhusiwa na polisi waliokuwa kwenye lango kuu la kuingilia, walidai wamepewa maelekezo ya kutoruhusu watu kuingia.
“Naomba usiingie ndani wala kupiga picha eneo hili, hayo ndiyo maelekezo ninayokupa na niliyopewa, vinginevyo mtafute RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa) akupe ruhusa,” alisema mmoja wa askari hao. Akizungumzia hali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo alisema polisi walikuwa wanatekeleza jukumu lao kwa umma la kulinda raia na mali zao kutokana na wananchi kwa makundi kusherehekea ushindi wa mteule huyo.
Konyo alisema ulinzi huo ulilenga kuweka na kuimarisha usalama kwenye makazi ya familia hiyo.
Hata hivyo, Konyo alipotakiwa kuzungumzia kuzuia watu kupiga picha kwenye makazi hayo alikata simu na hata alipopigiwa tena hakupokea.
Nyumbani kwake, Ada Estate, ulinzi ulianza kuimarishwa mara tu baada ya kiongozi huyo kutangazwa kuwa mgombea wa urais kupitia CCM.
Mmoja wa walinzi hao ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema wameongezwa walinzi wengine wanne mara baada ya matokeo ya mjini Dodoma kutangazwa.
Magari kadhaa yenye namba za serikali na magari ya polisi yalionekana yakiingia na kutoka nyumbani kwa Magufuli.
Kadhalika kama ilivyokuwa Chato, walinzi hao walisema wamepewa amri kutoruhusu watoto au mwanafamilia yeyote kutoka nje au kuzungumza na waandishi wa habari.MWANANCHI.

No comments