POLISI YATOA MIL.50/- KUWANASA WAUAJI.
SIKU moja baada ya tukio la kuuawa kwa watu saba wakiwemo askari wanne katika Kituo cha Polisi Stakishari, Ukonga jijini Dar es Salaam, Jeshi la Polisi nchini limetangaza donge nono la Sh milioni 50 kwa watakaofanikisha kukamatwa kwa wahusika wa tukio hilo.
Mbali ya mauaji, watu waliovamia kituo hicho walivunja ghala la silaha na kupora bunduki za kivita ambazo idadi yake haijafahamika, lakini ikikisiwa kuwa ni zaidi ya 15.
Aidha, mmoja wa askari aliyenusurika kifo licha ya kupigwa risasi za kifuani, amesimulia tukio hilo na kusema halikuwa la kawaida na kwamba watu waliowavamia kituoni walikuwa zaidi ya majambazi.
Sh milioni 50
Kutolewa kwa kiasi hicho cha fedha kumeelezwa kunakwenda sambamba na dhana ya Polisi Jamii na ulinzi shirikishi, hivyo kumfanya Inspekta Jenerali wa Polisi, IGP Ernest Mangu kuagiza wananchi washirikishwe katika suala hilo linalohusu ulinzi na usalama wa mali zao na Watanzania kwa ujumla.
Akizungumza jana ofisini kwake, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova alisema, yeyote atakayetoa taarifa za wahalifu hao atazawadiwa kitita hicho huku ikibaki kuwa ni siri kati ya Polisi na mtoa taarifa.
Aidha, alisema kutokana na tukio hilo, kuna mpango wa kuweka kamera za usalama katika vituo vya Polisi, ili kuweka kumbukumbu za watu wanaoingia na kutoka hata kama ni wahalifu iwe rahisi kupatikana.
“Tumeona ni bora kuongeza kiwango cha tahadhari na ulinzi katika vituo vya Polisi na maeneo mengine. Kwa hiyo mtu asije akaenda kituoni akashangaa kuona anachukua muda mrefu kuhudumiwa na anakaguliwa sana, hiyo kwa sasa ni kawaida,” alisema Kova.
Kova alitaka wananchi wasiwe na hofu na Jeshi la Polisi kwa kudhani limelegea, bali watoe ushirikiano kwa taarifa ili wahalifu hao waweze kutiwa mbaroni.
Hata hivyo Kamishna Kova alisema, Jeshi la Polisi limekubaliana kutotoa taarifa ambazo baadhi yake zinaweza kuleta hamaki kwa wananchi, kwani lengo siyo kuwatisha wananchi bali kushirikiana nao na kuhakikisha kuwa wahalifu na silaha zilizoporwa zinapatikana.
“Unajua unaweza ukasema labda zimeibwa silaha na mabomu ukawapa hofu wananchi kwa kudhani hawako salama, hivyo tumeona siyo kila taarifa ni ya kuiweka wazi ili kuweka tahadhari kwa wananchi,” alisema.
Aidha, alitaka yeyote atakayekuwa na taarifa awasiliane na yeye mwenye kwa namba 0754 034 224, Msemaji wa Polisi Advera Bulimba 0713 631 667 na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Diwani Athuman kwa namba 0715 323 444 au kuonana na viongozi wa makao makuu ya Polisi na Kanda Maalumu ana kwa ana.
Alisema pia wanaendelea na msako mkali wa kubaini maovu mbalimbali katika jamii ili kupambana na uhalifu wa aina zote ikiwemo ujambazi wa kutumia silaha, pamoja na makosa yote yanayoashiria uvunjifu wa amani.
Hatua hiyo inatokana na tukio la uvamizi wa Kituo cha Polisi cha Stakishari kilichopo Ukonga katika Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam na kuwaua askari wanne na raia watatu.
Simulizi la aliyejeruhiwa
Wakati Jeshi la Polisi likitangaza zawadi nono kwa watakaofanikisha kukamatwa kwa wahusika wa uvamizi na mauaji ya askari wa Stakishari, mmoja wa maaskari aliyenusurika kifo, Gaston Shadrack amesimulia tukio hilo akiwa wadi ya Kibasila katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam na kusema watu waliowavamia walikuwa zaidi ya majambazi, akiwafananisha na tukio la kigaidi.
Anasema: “Mimi naamini kabisa wale hawakuwa majambazi wa kawaida kwa sababu majambazi huwa wanakuwa na bunduki moja au mbili pamoja na mapanga labda na shoka, lakini wale walikuja wote wakiwa na bunduki mkononi, walikuwa ni watu wa hatari sana.”
Mbali na hilo, Shadrack aliyejeruhiwa sehemu za kifua na bega, alisema licha ya kujeruhiwa, alifanikiwa kumpiga risasi na kumuua jambazi anayeonekana katika picha zilizosambazwa katika mitandao mbalimbali mwenye ndevu.
Akielezea tukio hilo askari huyo alisema juzi akiwa askari wa zamu na wenzake katika kituo cha Stakishari lilikuja kundi la watu waliokuwa wamevaa makoti huku wakibishana mithili ya watu waliodhulumiana.
“Nilipowaona na zile kelele zao maana walikuwa kama watu nane hivi…..niliwazuia nje ya uzio wa kambi wasiingie ndani, ghafla wenye makoti yao wote walitoa bunduki na kuanza kutumiminia risasi, kwa bahati mimi zilinichuna kifuani na begani upande wa kulia nilidondoka na bunduki yangu,” alisema.
Alisema baada ya yeye kuanguka, majambazi waliamini amekufa hivyo kuingia ndani ya kituo cha Polisi na kuwamiminia risasi watu waliokuwa mapokezi ambao walikuwa ni askari wawili na wananchi waliokwenda kuripoti matukio.
Aidha alisema wakiwa huko ndani, jambazi mmoja (aliyemuua) walimwacha nje kwa ajili ya kuwalinda wenzake, ghafla alisikia ngurumo za pikipiki, akageuka kuangalia ndipo akafanikiwa kuinuka huku akiwa na maumivu makali kwa kutumia bunduki iliyokuwa pembeni yake kumpiga risasi mbili jambazi huyo.
“Nilijitahidi nikakimbia na kwenda kujilaza kwenye shamba la mahindi nikiwa nimejificha, nilisikia milio ya risasi ikiendelea kulia na baadaye kidogo niliwasikia wakiondoka na pikipiki zao, niliinuka na kurudi kituoni,” alisema Shadrack na kuongeza kuwa, alishuhudia miili ya wenzake na raia waliopigwa risasi, kabla ya kuishiwa nguvu na kukimbizwa kituo cha afya Arafa cha Ukonga na baadaye Hospitali ya Amana, Ilala.
Alisema watu walionusurika ni pamoja na askari mwenzake mmoja wa kike ambaye wakati majambazi wakiingia yeye alikuwa kwenye chumba cha wapelelezi pamoja na wanawake wengine wawili ambao ni raia wa kawaida kwa sababu majambazi hao hawakufika huko zaidi ya chumba chenye silaha na kuchukua silaha na kuondoka.
Aidha alisema hawezi kuhisi ni watu gani ambao walitoa taarifa za silaha zilizokuwepo katika kituo hicho kwa sababu vituo vya Polisi ni sehemu ambayo wanakwenda watu mbalimbali kwa ajili ya malalamiko na matatizo yao.HABARI LEO
Post a Comment