Header Ads

MWENYEKITI ATUPWA JELA KWA KULINDA MKULIMA WA BANGI.

MAHAKAMA ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa imemhukumu Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbende, Alei Charles (Chadema) kifungo cha miaka miwili jela baada ya kukiri kumlinda mshtakiwa Wenceslaus Namwanda “Pepea” anayemiliki shamba la bangi.
Mshitakiwa Namawanda ambaye pia ni mkazi wa kijiji cha Mbende anakabiliwa na kosa la kumiliki shamba la bangi.
Hakimu wa mahakama hiyo, Adam Mwanjokolo alitoa adhabu hiyo baada ya mshtakiwa huyo mwenye miaka 30 kukiri kutenda kosa hilo mahamakani hapo .
“Nimelazimika kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa viongozi wengine wenye tabia kama yako (Alei)… hivyo utatumikia kifungo cha miaka miwili jela,“ alisema Hakimu Mwanjokolo.
Awali Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi wa Polisi, Hamimu Gwelo alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Mei 14 , mwaka huu katika kijiji cha Mbende , saa 3 usiku.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa usiku huo wa tukio Alei aliwadanganya maofisa wa polisi kuwa mshtakiwa Namwanda hakuwa mkazi wa kijiji hicho hivyo aliwaelekeza kwa Mwenyekiti wa kijiji cha jirani.
Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka, maofisa hao walithibitishiwa na Mwenyekiti wa kijiji cha jirani kuwa mshitakiwa wanayemtafuta anaishi katika kijiji cha Mbende ambapo aliongozana nao hadi nyumbani kwake.
“Maofisa wa Polisi walipofika nyumbani kwa mshtakiwa Namwanda walipobisha hodi ghafla alitoka mtu baada ya kuona askari alitimua mbio, askari walifanikiwa kumkamata na ikagundulika kuwa ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbende ambapo alikiri kuwa alifika nyumbani kwa mshtakiwa na kumtaarifu atoroke kwa kuwa alikuwa akitafutwa na Polisi,” alieleza Mwendesha Mashtaka.
Akijitetea mshitakiwa huyo aliomba apunguziwe adhabu kwa kuwa ni kosa lake la kwanza. Pia ana watoto wategemezi wawili wa marehemu dada yake ambapo mama mzazi anaishi naye baada ya mumewe kufariki dunia.HABARI LEO.

No comments