Header Ads

LIPUMBA AMNADI MAKONGORO NYERERE.


Image result for LIPUMBA
KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) anayewania urais, Makongoro Nyerere, ‘amekuna’ viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kiasi cha Mwenyekiti wa umoja huo, Profesa Ibrahim Lipumba, kumtaja kama jasiri wa kufichua vibaka ndani ya chama hicho tawala.
Ukawa unaundwa na vyama vinne vya upinzani ambavyo ni Chama cha Wananchi (CUF) kinachoongozwa na Profesa Lipumba, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), National Convention for Construction and Reform (NCCR - Mageuzi) na National League for Democracy (NLD).
Makongoro ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ni miongoni mwa wanachama 41 wa CCM waliochukua fomu za kuomba kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro cha urais wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu.
Profesa Lipumba alimmwagia Makongoro pongezi hizo wakati akihutubia umati mkubwa wa watu katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Mbugani jijini Mwanza, mwishoni mwa wiki iliyopita.
"Makongoro Nyerere aliwaeleza ukweli kwamba CCM kimekamatwa na vibaka... hawa vibaka hawaondoki hivi hivi mpaka waondolewe," alisema Profesa huyo wa uchumi na mwanasiasa maarufu nchini.
Akitangaza nia ya kugombea urais nyumbani kwao katika kijiji cha Mwitongo, Butiama mkoani Mara Juni mosi, mwaka huu, Makongoro alisema CCM kinawavunja moyo wanachama wake na kuwakatisha tamaa Watanzania kutokana na 'kubakwa na vibaka' huku akijinadi kuwa ndiye mwenye uwezo wa kuwarudishia matumaini.
"Sisi ndio wazalendo, tunasema mnapotaka kutupora hiki chama sisi tupo, turudishieni na mnapotaka kuturudishia kipitishie kwa Makongoro Nyerere, mna uhakika chama hiki hakipotei, siyo kumkabidhi kibaka.
"Ni kujidanganya kusema hakuna vibaka ndani ya CCM wakati wapo na wanatumia fedha zao, nyingine walizozipata kwa wizi kukivuruga chama," alisema Makongoro.
Kitendo cha kiongozi wa Ukawa, Profesa Lipumba, kumpongeza Makongoro hadharani ni dhahiri kimesaidia kumpiga jeki ya kisiasa kada huyo wa CCM katika harakati zake za kuusaka uongozi wa nchi miongoni mwa wenzake wengi wenye nguvu ya fedha na madaraka makubwa serikalini.
Hata hivyo, Profesa Lipumba alisema CCM kimefika hatua ambayo hakiwezi kuleta mabadiliko ya kuboresha maisha ya Watanzania kutokana na kuelemewa na wimbi la mafisadi wanaokitumia kufuja fedha za umma kujinufaisha na familia zao binafsi.
Aliendelea kukumbusha kwamba umaskini unaowakabili Watanzania hautokani na laana ya Mungu, bali ni matokeo ya uongozi mbovu wa CCM ulioweka kando tunu za muhimu za uwajibikaji, uwazi na uadilifu.
Katika mkutano huo uliotawaliwa na utulivu mkubwa, Profesa Lipumba aliwaomba Watanzania kuhakikisha wanatumia vizuri Uchaguzi Mkuu ujao kwa kuchagua Ukawa kuongoza nchi kwa ajili ya kuleta mabadiliko chanya ikiwa ni pamoja na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha na mali nyingine za umma.
"Tuwachague Ukawa waijenge nchi, mambo haya yanawezekana tukiwa na uongozi unaowajibika, uongozi wa uwazi na wenye maadili. Matatizo ya nchi yetu ni ya uchumi, ajira na matumizi mabaya ya fedha za umma. Tunahitaji mabadiliko ya kukidhi mahitaji ya wananchi," alisema.
Aliahidi kwamba Ukawa ukikabidhiwa uongozi wa nchi utakakikisha pamoja na mambo mengine, kunakuwepo na sera ya makusudi ya kuongeza ajira nchini ili kurejesha matumaini kwa vijana waliokata tamaa ya maisha kutokana na kukosa ajira.
"Tunataka rais atakayekuwa na huruma kwa Watanzania, baadhi ya vijana wa Tanzania wamekata tamaa kwa kukosa ajira. Matatizo yanasababisha vijana kuzeeka kabla ya wakati, lazima tuwe na sera ya makusudi ya kuongeza ajira," alisema na kufafanua kuwa juhudi kubwa zitaelekezwa katika kuwekeza kwenye viwanda ili kufanikisha lengo hilo.
"Viwanda vya kusindika mazao mbalimbali vitasaidia kujenga ajira, lakini inahitajika serikali makini na umeme wa uhakika. Rasilimali za bandari, utalii na gesi asilia nazo zikitumika vizuri zitaongeza ajira," alisema.
Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, kitendo cha wabunge wanachama wa Ukawa kususia vikao vya Bunge Maalum la Katiba (BMK) kutokana na baadhi ya maoni ya wananchi kuchakachuliwa, ni miongozi mwa viashiria vinavyodhihirisha kwamba umoja huo una uwezo wa kuongoza nchi kwa tija.
"Tumeshawishi bungeni kutetea maoni ya wananchi hadi tukaacha posho bungeni, tulikubali njaa ya matumbo yetu tukakataa njaa ya akili zetu," alisema na kutaja maoni ya wananchi yaliyoondolewa kwenye Katiba Inayopendekezwa kuwa ni pamoja na Tunu za Taifa alizozitaja kuwa ni Uwajibikaji, Uwazi na Uadilifu.
"Pia kifungu cha kupiga marufuku kiongozi kuwa na akaunti ya fedha nje ya nchi nacho kilinyofolewa katika Katiba Inayopendekezwa," aliongeza Mwenyekiti huyo wa Ukawa.
Kauli hiyo ya Profesa Lipumba kuhusu maoni ya wananchi juu ya Katiba Mpya ni tafsiri ya moja kwa moja kwamba Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba, alikusudia kukisaficha CCM dhidi ya kashfa zinazokiandama kutokana na msimamo wake wa kutetea tunu hizo za Taifa na kifungu hicho cha kuzuia kiongozi kuwa na akaunti nje ya nchi, miongoni mwa vingine kadhaa.
Mafisadi papa, sangara kukiona
Huku akiahidi kumuunga mkono kada mwenzake atakayeteuliwa kuwakilisha Ukawa katika kinyang'anyiro cha urais ikiwa yeye atapungukiwa vigezo, Profesa Lipumba alisema kipaumbele cha kwanza cha serikali itakayoundwa na umoja huo ni kuwakamata na kuwatupa jela mafisadi na wala rushwa wakubwa.
"Tukiingia madarakani jambo la kwanza ni kuyakamata mapapa na masangara ya ufisadi wa Tegeta Escrow na kuyafikisha mahakamani. Lazima mapapa na masangara ya ufisadi yaende jela ndipo dagaa wa ufisadi waogope," alisema na kushangiliwa mkutanoni.
Alisisitiza "Wito wetu kwa wananchi ni mafisadi waende jela, siyo kuchukua fomu kugombea urais... hili ni jambo la msingi katika kupambana na rushwa na ufisadi. Ukitaka kupambana na ufisadi katika miezi sita ya kwanza (ya serikali ya Ukawa), lazima mafisadi wakubwa waende jela".

No comments