Mkuu wa shule amzaba kofi mwalimu mbele ya wanafunzi
Katika hali isiyo ya kawaida Mkuu wa Shule ya Sekondari Kabwe iliyoko mwambao mwa Ziwa Tanganyika, Nkasi mkoani Rukwa, Jackson Mussa, amemtandika kofi mwalimu mwenzake, Emmanuel Mbemba, mbele ya wanafunzi wake.
Akizungumzia tukio hilo, Mratibu Elimu Kata ya Kabwe, Geofrey Mtafya, alisema tukio la kupigwa kofi mwalimu huyo, lilitokea juzi asubuhi majira ya saa 4:00 asubuhi na kusababisha taharuki kubwa kwa wanafunzi na walimu wengine wa shule hiyo.
Mtafya alisema siku ya tukio hilo, Mwalimu Mbemba alikwenda ofisini kwa Mkuu wa shule kuomba ruhusu ili awapeleke wanafunzi kwenye ziara ya mafunzo kwa kutembelea fukwe za Ziwa Tanganyika.
Mkuu huyo wa shule alimtaka mwalimu huyo aandike barua ya kiofisi na alifanya hivyo. Aliipokea barua hiyo na kumwahidi mwalimu huyo kuwa baada ya muda si mrefu atampatia majibu kwa maandishi.
Alisema baada ya kusubiri kwa muda bila majibu, Mwalimu Mbemba ambaye anafundisha Kidato cha tatu somo la Jiografia, alimfuata mkuu wake wa shule na kumkumbusha kuwa bado anasubiri. Mkuu wa shule alijibu kuwa alikuwa bado hajaandika barua ya ruhusa kwa kuwa alikuwa na majukumu mengine.
Baada ya muda mrefu tena kupita, mwalimu huyo wa Jiografia alimfuata Mkuu wa Shule ikiwa ni mara ya tatu na kumweleza kuwa anachelewa kwenda kwenye ziara ya mafunzo na wanafunzi, kitendo kilichomkasirisha mkuu huyo wa shule, ndipo alipomfuata na kumkaba koo Mwalimu Mbemba mbele ya wanafunzi na akaanza kumzaba vibao mfululizo.
Taarifa kutoka shuleni hapo zinaeleza kuwa wanafunzi wa shule hiyo walishuhudia tukio hilo huku baadhi yao walianza kupiga kelele hatua iliyosababisha walimu wengine kwenda kuamua na kuwaachanisha walimu hao waliokuwa wamekwidana mashati.
Mwalimu Mbemba alitoa taarifa kwa kiongozi wa Chama Cha Walimu (CWT) mahali pa Kazi, Elia Elia ambaye alimwarifu Ofisa Mtendaji Kata ya Kabwe, Geoffrey Kuzumbi ambaye aliitisha kikao cha dharura shuleni hapo.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa Mkuu wa Shule huyo alikana kumpiga kofi mwalimu mwenzake bali alidai kuwa alimkaba koo tu. Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Nkasi, Abel Ntupwa, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kukemea kitendo hicho kuwa ni utovu wa nidhamu huku akiahidi kutolea uamuzi wiki ijayo baada ya kupatiwa ripoti kamili.
Post a Comment