Mwalimu wa Sekondari Ajinyonga kwa Kunywa Sumu
Mwalimu Betson Sanga aliyekuwa akifundisha Shule ya Sekondari Milundikwa wilayani Nkasi amefariki dunia baada ya kunywa sumu akiwa katika nyumba ya kulala wageni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema mwalimu huyo alifariki dunia juzi usiku huku akiwa ndani ya chumba alichokuwa amepanga karibu na kituo kikuu cha mabasi yanayokwenda mikoani.
Alisema hadi sasa hajafahami chanzo cha mwalimu huyo kujiua kwa sumu ingawa aliacha ujumbe uliosomeka, “Kama nadaiwa deni lolote na mtu amweleze mkurugenzi ambaye ni mwajiri wangu lakini asilaumiwe, nisilaumiwe chochote juu ya kifo changu”.
Inadaiwa kwamba siku ya tukio mwalimu huyo alifika katika nyumba hiyo ya kulala wageni na kupanga chumba kwa ajili ya kulala na baadaye alikabidhi funguo na kuondoka kwenda kusikojulikana.
Taarifa zinadai ilipofika usiku wa manane alirejea katika nyumba hiyo akiwa amelewa akachukua ufunguo kwa mhudumu na kuingia ndani ya chumba chake kulala.
Baada ya muda mhudumu wa nyumba hiyo alisikia sauti ya mtu akikoroma kwa sauti ya juu hali iliyzua hofu.
Mhudumu alilazimika kuomba msaada kwa wapangaji wengine waliokuwamo ndani ya nyumba hiyo na kuvunja mlango.
Baada ya kuvunjwa kwa mlango mhudumu huyo akiwa na wapangaji hao, walimkuta mwalimu huyo akiwa anatokwa mapovu hali iliyowalazimu kumkimbiza hospitalini lakini wakiwa njiani alifariki dunia.
RPC Kyando alisema kwa mujibu wa uchunguzi wa utabibu, Mwalimu Sanga alikunywa sumu.
Post a Comment