Katibu wa Mbunge wa Geita Mjini ,Mariam Mkaka akiwasisitiza wanafunzi hususani ni wa kike kusoma kwa Bidii zaidi kutokana na kwamba serikali imetatua changamoto yao kwa kujenga Mabweni.
Picha zote na Joel Maduka wa Maduka Online.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja Jenereli Mstaafu Ezekiel Kyunga amezindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mitano ambapo mitatu ni vituo vya afya na viwili ni shule moja na Mabweni kwenye shule ya sekondari Kasamwa.
Akielezea Miradi hiyo yote Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mhandisi Modest Aporinali amesema bajeti ambayo waliyonayo kwa kila kituo cha afya wametenga kiasi cha sh ,Milioni Mia moja na kwamba mahitaji ni vituo vya afya kumi na kwasasa ni vituo viwili ambavyo vinafanya kazi.
“Ni kweli Halamshauri yetu ina uhitaji mkubwa sana wa Vituo vya afya ingawa kwa sasa tunavyo vituo viwili ambavyo ni Nyankumbu na Kasamwa ambavyo vinafanya kazi, hata hivyo mmeona tumezindua na kuweka mawe ya msingi kwenye vituo vitatu ambapo ni Mpomvu,Nyanguku na Shiloleli tutaendelea na jitihada kwa kutumia mapato yetu ya ndani ili kupunguza changamoto ya vituo vya afya hata hivyo GGM wametupa msaada kama milioni mia moja kwaajili ya ujenzi wa kituo cha afya Mgusu”Alisema Modest.
Hata Hivyo Mkurugenzi Modest ametaja miradi ya shule ambazo zimewekewa mawe ya msingi kuwa ni shule ya Msingi Tumaini pamoja na Mabweni kwenye shule ya sekondari Kasamwa na kwamba wanaendelea na juhudi ya kupambana na changamoto za elimu kwenye Halmashauri ya Mji.
Mkuu wa Mkoa ,Meja jenerali mstaafu Ezekiel Kyunga ,amesisitiza kuwa serikali inafanya juhudi za kuwashirikisha wananchi katika swala la maendeleo na kwamba wanatakiwa kuwa na mwitikio katika swala la maendeleo kwa wao kama wananchi kwa kujitolea bila ya kusubiria serikali huku akiwataka baadhi ya watu kutokuwa na desturi ya kulalamika bila ya kufanya shughuli kwa kushirikiana na Serikali.
Jumla ya miradi yote ambayo imezinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi imeghalimu kiasi cha Sh,Milioni Mia saba na thelasini na sita pesa ambazo zinatokana na mapato ya ndani.
|
Post a Comment