JELA,VIBOKO KWA KUMBAKA MWANAFUNZI.
Maswa. Tukio la kumbaka na kumtorosha mwanafunzi mwenye umri wa miaka 15 limemtokea puani Gervas Elihuruma (20), ambaye sasa atatumikia miaka 30 gerezani.
Sanjari na adhabu hiyo, pia jamaa huyo amechapwa viboko 12 baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanafunzi huyo.
Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Fredrick Lukuna baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashtaka.
Akitoa hukumu dhidi ya Elihuruma, mkazi wa Kijiji cha Sangamwalugesha wilayani hapa, Hakimu Lukana alisema adhabu hiyo imelenga kutoa fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kutenda kosa kama hilo.
Awali, ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka Mkaguzi wa Polisi, Nassib Swedy kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Septemba 20, 2016 saa saba mchana kijijini hapo.
Swedy aliieleza Mahakama kuwa mshtakiwa alimrubuni na kumbaka mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 15 ambaye alikuwa anasoma darasa la sita katika Shule ya Msingi Sangamwalugesha.
Mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa mshtakiwa baada ya kumbaka mwanafunzi huyo alimtorosha na kwenda naye mjini Kateshi mkoani Manyara kuishi naye kama mkewe kwa takribani mwezi mmoja.
Kabla ya hukumu hiyo, Swedy aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili liwe fundisho kwa wengine wenye tabia ya kuwaharibia masomo wanafunzi.
Akizungumzia adhabu za ubakajil Isaiah Buzungu alisema: “Ingekuwa adhabu kama hizi zinapotolewa zinatangazwa redioni kila mara, nadhani lingekuwa jambo jema sana.”
SOURCE:MWANANCHI
Post a Comment