Header Ads

Askari polisi afariki ghafla kituoni

ASKARI mmoja wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza,  amefariki ghafla akiwa eneo la kazi katika kituo cha Polisi Nyagezi, jijini Mwanza.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi,  alimtaja askari huyo kuwa ni Koplo Marco Mahona,  ambaye alifariki juzi saa saba  mchana wakati akitekeleza majukumu yake.

Akielezea jinsi kifo hicho kilivyotokea, Kamanda Msangi alisema,  Koplo Mahona akiwa ndani ya ofisi iliyopo eneo la stendi ya mabasi yaendayo mikoani ya Nyegezi,  alisikia sauti za wananchi waliokuwa eneo hilo wakimzomea mwanamke ambaye alikuwa anapita karibu na kituo  akiwa na watoto wake ndipo alinyanyuka kuangalia ili kujua tatizo ni nini.

Alisema wakati akiwa karibu na mlango wa kituo hicho akiwa na lengo la kusogea eneo ambalo wananchi wanamzomea mwanamke huyo, ghafla alianguka na  kupoteza maisha.

“Kwa mujibu wa mashuhuda mwanamke huyo wakati anazomewa  huku akirusha mikono juu ikiwa ni ishara ya kuwaambia  waachane naye, sasa  kwa kuwa kazi ya askari polisi ni usalama wa raia ilimlazimu  askari wetu kutoka nje ili aweze  kujua kinachoendelea.

“Lakini kwa bahati mbaya alipotoka tu nje alianguka akapoteza fahamu na baada ya kupelekwa hospitali  na kubainika  kwamba amepoteza maisha,  mwili wake upo katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi ili tubaini sababu za kifo chake.

“Lakini cha kusikitisha ni kwamba tangu  baada ya tukio hili kutokea baadhi ya wananchi wamekuwa wakisema mambo mbalimbali ambayo hayana ukweli.

No comments