Header Ads

Mvua yaibua hofu ya njaa Mbeya

Wananchi mkoani Mbeya wameanza kushuhudia mvua chache zikinyesha, huku zikiwa zimechelewa katika maeneo mengi na kusababisha wakulima kuishi kwa hofu ya kukumbwa na njaa.

Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Issa Hamad amesema utabiri huo bado unaendelea na kwamba, mvua itaendelea kunyesha chini ya kiwango katika maeneo mengi.

Ametoa kauli hiyo wakati wakazi wa mkoani hapa kwa miaka mingi wamezoea kusherehekea sikukuu ya Krismas wakati mahindi yakiwa na urefu wa futi mbili na nusu hadi tatu, lakini mwaka huu wamesherehekea sikukuu hiyo mahindi yakiwa hayajapandwa.

Mkulima wa Kijiji cha Igalako wilayani Mbarali, Bedon Mwakitalima amesema kwa kawaida wanapanda mahindi Novemba, lakini  hadi jana walikuwa hawajapanda kwa kukosa mvua.

“Desemba hii ndiyo tungeotesha mbegu za mpunga kwenye vitalu, lakini mpaka sasa bado kwa sababu ya jua kali,’’amesema.


Mkulima mwingine wa Kijiji cha Inyala, Ngalele Edward amesema kwa kawaida mvua huanza kunyesha Agosti na Septemba kazi ya kupanda viazi mviringo na mahindi huanza tofauti na mwaka huu.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Lugombo wilayani Rungwe, Andrew Kalulu amesema mvua kunyesha kidogo, hali hiyo imewaweka njiapanda wakulima wengi ambao mpaka sasa hawana uhakika wa mavuno.

Katibu Tawala Msaidizi mkoani Mbeya anayeshughulikia Kilimo, Chibagu Nyasebwa amesema kwa kawaida mvua nyingi huanza kunyesha Oktoba hadi Novemba  tofauti na mwaka huu, jambo lililosababisha kamati ya ushauri ya mkoa kupanga mikakati ya kuwasaidia wakulima.

Meneja wa TMA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Issa Hamad  ameshauri wananchi kutengeneza miundombinu ya kuvuna maji kwani kuna uwezekano wa mvua kukatika mapema.

No comments