Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Lataka Mmiliki wa Jamii Forums Aachiwe Mara Moja.
Kwa muda wa siku tatu sasa Jeshi la Polisi Tanzania linamshikilia Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jamii Media Limited, Maxence Melo katika Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Dar es Salaam.
Hadi sasa, si Melo, familia yake au wanasheria wake walioelezwa kosa linalomfanya ashikiliwe. Wanasheria wa Melo wameweka kambi katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, lakini hakuna majibu ya maana wanayopewa na wala Melo hafikishwi mahakamani.
Taarifa wanazotoa askari waliopo kituoni hapo, ambazo si taarifa rasmi, ni kwamba Melo anashikiliwa kwa nia ya kumtaka awape polisi majina wanayoyahitaji ya wachangiaji wa masuala mbalimbali katika mtandao wa Jamii Forums kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandaoni huku wakidai ni maelekezo kutoka “juu”.
Siku ya Jumatano, Desemba 14, 2016 polisi wamefika ofisini na nyumbani kwa Melo wakapekua sehemu zote. Taarifa kutoka ofisini kwa Melo zinaonyesha polisi wamechukua nyaraka mbalimbali ikiwamo hati ya kusajili kampuni, leseni ya biashara na nyingine.
Pia polisi wameondoka na wafanyakazi wawili wa Kampuni ya Jamii Forums kwa mahojiano zaidi.
Taarifa nyingine zinaonyesha kuwa polisi wanaomshikilia Melo wanajiapiza kuwa hata kama mawakili wake watakwenda mahakamani hawatamwachia hadi atekeleze wakitakacho.
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) linafuatilia kwa karibu mwenendo na utendaji wa Jeshi la Polisi juu ya suala la uhuru wa kujieleza na kutoa maoni unaotolewa na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977).
Katika siku za karibuni, TEF na Watanzania kwa ujumla wanashuhudia ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na Jeshi la Polisi linaloelekea kuacha kuheshimu misingi ya utawala wa Sheria na Katiba ya Tanzania.
Melo kama mtuhumiwa anayo haki ya kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma katika muda usiozidi saa 24. Kitendo cha polisi kumshikilia kwa siku tatu, ambapo hatujui kama anateswa au la, ni uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu.
Tamko la Haki za Binadamu la Mwaka 1948 linavitaka vyombo vya dola kuheshimu utawala wa sheria ambao pamoja na mambo mengine msingi wake ni kuheshimu mgawanyo wa madaraka (separation of power). Kitendo cha Polisi kuanza kuchukua sheria mkononi kwa kukamatakamata watu, kuwatisha waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu hakikubaliki.
TEF inalitaka Jeshi la Polisi kumwachia mara moja Melo bila masharti au kumfikisha mahakamani na kumfungulia mashitaka kwa mujibu wa sheria ikiwa ana kosa.
Tunamwomba Rais John Magufuli aingilie kati mzozo huu na kuwafahamisha polisi kuwa wanayoyatenda wanapalilia mbegu ya chuki katika nchi jambo ambalo si jema waliache mara moja.
TEF inaungana na Watanzania kulaani kitendo cha polisi kumkamata Melo kwa kutumia sheria mbaya isiyokubalika ya Makosa ya Mtandaoni.
TEF inatetea haki ya uhuru wa kutoa mawazo na kukataa ukandamizaji huu wa polisi wanaodai wana maelekezo kutoka juu chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano. Mungu ibariki Tanzania.
Theophil Makunga,
Mwenyekiti,
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
Dar es Salaam, Desemba 15, 2016
Post a Comment