Rais wa Burundi amesaini rasmi kuiondoa nchi hiyo katika Mahakama ya ICC
Baada ya Serikali ya Burundi kutoa taarifa ya kutaka kujiondoa kwenye Mahakama ya makosa ya jinai ICC, Hatimaye imetoka Ripoti kuhusu Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi kusaini mkataba wa kuiondoa nchi yake katika Makahama ya Kimataifa ya Jinai ICC.
Kutiwa saini mkataba huo na Rais Nkurunziza kunamaanisha kujiondoa taifa la Burundi katika mkataba wa Roma ambao ndio uliunda mahakama hiyo ya jinai. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, awali tarehe 12 ya mwezi huu bunge la Burundi lilipasisha muswada wa kujiondoa nchi hiyo kutoka mahakama ya ICC.
Itakumbukwa kuwa Burundi ilitia saini mkataba wa Roma mwezi Januari mwaka 1999 huku ikiupashisha mnamo mwaka 2004. Aidha hatua hiyo ya Rais Nkurunziza hapo jana, inaifanya Burundi kuwa nchi ya kwanza kujiondoa kwenye mahakama hiyo.
Serikali ya Bujumbura inaituhumu Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kuwa ya kisiasa na ambayo ipo kwa ajili ya kuzikandamiza nchi za Kiafrika pekee.
Mbali na Burundi, nchi kadhaa za Kiafrika zimetishia kujiondoa kwenye mahakama hiyo kutokana na hatua yake ya kuendelea kuwasakama viongozi wa nchi za bara hilo, huku ikifumbia macho jinai zinazofanywa na mataifa waitifaki wa Magharibi.
Post a Comment