Header Ads

Madaktari wagoma kuripoti kazini,hopitali ya Ligula Mtwara.


Licha ya Wizara ya Afya na ustawi wa jamii kuwapangia madaktari nane kuripoti kazi katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ligula ni madaktari watatu tu ndiyo wameripoti mpaka hivi sasa,huku ikiwa imepita miezi sita madaktari watano hawajaripoti hali inayochangia utendaji wa kazi kuwa mgumu.

Hatua ya kuripoti madaktari hao imekuja baada ya wizara ya afya kuwahamisha madaktari kumi na mbili wa hospitali ya mkoa ya Ligula na kuwahamishia madaktari wapya 8 katika hospitali ya Ligula lengo likiwa kuboresha utendaji wa kazi.

Akizungumza na ITV/RadioOne Mganga Mkuu wa hospitali ya mkoa wa Ligula Saini Diksoni amesema licha ya serikali kuwa na nia njema ya kuboresha utendaji wa kazi katika hospitali hiyo ni madaktari watatu tu ndiyo wameripoti kazi.
Amesema hali hiyo imekuwa ikichangia madaktari wachache waliyopo kufanya kazi pasipo kupumzika na hivyo kuchangia utendaji wa kazi kuwa mgumu.

Akizungumzia hali hiyo,mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego amesema ofisi yake imekuwa ikiwasiliana na wizara ili kuona changamoto hiyo inatatuliwa huku akisisitiza madaktari waliyopangiwa katika hospitali hiyo kuripoti kazini.

CHANZO:ITV

No comments