Header Ads

Mlinzi wa Wizara ya Ujenzi atupwa jela miaka mitatu Kwa Kosa la Kushindwa Kuzuia Wizi wa Kiti na Kompyuta


Mkazi wa Temeke Ramadhani Kusena (48) amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana na hatia ya kushindwa kuzuia wizi usitokee katika Wizara ya Ujenzi, wakati akiwa mlinzi wa eneo hilo. 

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Catherine Kioja alisema jana kuwa mahakama imemtia hatiani mshtakiwa huyo baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wanne. 

Mbali na kifungo hicho, mahakama pia imemuamuru mshtakiwa huyo kulipa fidia ya Sh500,000 kwa kushindwa kuzuia wizi wa kiti na kompyuta katika chumba namba 303 kilichopo katika ofisi za wizara hiyo. 

Hakimu Kioja alisema mshtakiwa huyo anaweza kukata rufaa kama ataona hajatendewa haki na mahakama hiyo katika hukumu hiyo. 

Awali, kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Grace Mwanga uliomba mahakama kutoa adhabu kulingana na shtaka hilo. Hata hivyo, Mahakama ilimpa nafasi mshtakiwa ajitete kwanini asipewe adhabu. 

Akijitetea, mshtakiwa huyo aliomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa anategemewa na familia. Wakili Mwanga alisema mshtakiwa alitenda kosa hilo Julai 7, 2014 katika ofisi za wizara hiyo Mtaa wa Samora Dar es Salaam. 

No comments