Header Ads

Takukuru wamdaka mtumishi hewa Bukombe


Bukombe. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inamshikilia mwalimu wa Shule ya Sekondari Butinzya, wilayani hapa Mkoa wa Geita kwa tuhuma za kupokea mishahara ya miezi 12 bila kufanya kazi.

Kamanda wa Takukuru wa Wilaya Bukombe, Shija Chuzela alisema wanamshikilia mwalimu huyo tangu Aprili 25, mwaka huu baada ya kubainika kuwa ni mtoro wakati wa uhakiki wa wafanyakazi hewa. “Tulipokea taarifa kuhusu utoro huu kutoka kwa maofisa wanaofanya kazi ya uhakiki baada ya mwalimu huyo kufika shuleni hapo kwa ajili ya kuhakiki taarifa zake,” alisema Kamanda Chuzela.

Alisema kabla ya kukamatwa, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Weneslaus Kalyango alikana kumfahamu mwalimu huyo na alipoitwa na wahakiki bado alimkana kwa madai kuwa tangu aliporipoti shuleni hapo Mei, mwaka jana hajaonekana mpaka juzi alipokwenda kwenye uhakiki. “Mwalimu huyo ni kati ya wale waliopata ajira mpya serikalini mwaka jana baada ya kuripoti shuleni hakuonekana tena, anadai eti alikwenda masomoni bila kibali cha mwajiri huku akiendelea kupokea mshahara bila kufanya kazi kwa mwaka mzima,” alisema.

Alisema baada ya kumkamata, Takukuru ilifanya uchunguzi kwa kukagua madaftari ya mahudhurio shuleni hapo na kujiridhisha kuwa hajaonekana kwa kipindi chote hicho. “Ndiyo maana hata Mkuu wa shule alishindwa kumtambua.”

Alisema baada ya uchunguzi imebainika mwalimu huyo alikuwa akipokea mshahara wa Sh716, 000 kila mwezi kwa kipindi chote alipokuwa mtoro.

Kitendo hicho kwa mujibu wa Kamanda huyo wa Takukuru, kimeitia hasara Serikali ya Sh8.5 milioni.

Alisema wanaendelea kumshikilia wakisubiri uchunguzi ukamilike ili afikishwe mahakamani ambako atalazimika kuzirejesha fedha hizo serikalini. 

No comments