Header Ads

Rais Magufuli Azindua Daraja la Kigamboni....Akataa Lisiitwe kwa Jina Lake, Ashauri Liitwe Daraja la Nyerere


Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John Magufuli amekataa daraja la Kigamboni  lisiitwe 'Daraja la Magufuli' na badala yake ameshauri lipewe jina la muasisi wa Taifa hili, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Akiongea wakati wa kuzindua daraja hilo leo, Rais Magufuli amesema kuwa awali aliletewa mapendekezo  na waziri mwenye dhamana akimtaka aridhie daraja hilo lipewe jina lake, lakini kwakuwa wazo la ujenzi huo lilianza tangu wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere, alikataa na  kushauri jina  la Nyerere litumike .
 
“Nilikataa lisiitwe kwa jina langu kwa sababu wazo  la ujenzi wa daraja hili lilianza  mwaka 1979 wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere.

"Wazo hilo halikufanikiwa kutokana na ukosefu wa pesa wakati huo. Mwalimu Nyerere ni kiongozi aliyejenga  misingi imara katika taifa letu.

"Alikuwa ni kiongozi asiyebagua mtu kwa misingi ya dini, chama au kabila. Alifanikiwa kutuunganisha watanzania wote bila kujali itikadi zetu.

"Leo hii, daraja hili limekamilika, ni daraja ambalo halitambagua mtu kwa sababu wa CCM watapita hapa, wa Chadema watapita hapa na bahati nzuri mstahiki Meya wa jiji hili  ambaye ni Chadema naye yuko hapa na amepita katika daraja hili.

"Ndugu zangu sistahili sifa zozote, najua nimefanikisha ujenzi huu  nikiwa waziri wa ujenzi, lakini wakati huo nilikuwa natimiza wajibu wangu kama mtumishi wa umma, hivyo nashauri hili daraja liitwe daraja la Nyerere ili tuweze kumuenzi  mwasisi wa taifa hili” alisema  Rais Magufuli.
 
Aidha Rais Magufuli amewataka wakazi wa jiji la Dar es Salaam kuhakikisha wanalitunza daraja hilo katika kujenga uchumi wa taifa.

No comments