Ofisi ya Waziri Mkuu Kutumia Bajaji na Bodaboda
Ofisi ya Waziri Mkuu itatumia usafiri wa bajaji na bodaboda kuendesha shughuli zake kuanzia mwaka ujao wa fedha wa 2016/2017 ikiwa ni mkakati wa kubana matumizi wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Mpango huo umo kwenye hotuba ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyosomwa jana bungeni na Kassim Majaliwa, na baadaye kusifiwa na mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge, Mohamed Mchengerwa wakati akisoma maoni ya kamati kuhusu bajeti hiyo.
Wizara iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni ya Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Walemavu.
Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo, Mchengerwa alisema uamuzi wa aina hiyo unaendana na dhana ya kubana matumizi ya fedha wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Hata hivyo, hotuba iliyosomwa na Waziri Majaliwa haijaeleza pikipiki hizo za magurumu mawili na matatu zitatumiwa na watumishi wa kada gani.
Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa kwenye mkakati mkali wa kubana matumizi yasiyo ya lazima na tayari Rais John Magufuli ametangaza kuwa kuanzia mwaka mpya wa fedha hakuna mtumishi wa umma atakayelipwa zaidi ya Sh15 milioni, huku akifuta sherehe za maadhimisho ya siku za kitaifa, zikiwamo za Muungano na Uhuru.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec)
Katika maoni yake, kamati hiyo imeitaka Serikali kutoa tamko kuhusu maandalizi na utekelezaji wa mchakato wa kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
Pia kamati hiyo ilitaka Nec kuweka utaratibu mpya wa ratiba ya upigaji kura ili chaguzi zote za rais, wabunge, madiwani na viongozi wa Serikali za mitaa zifanyike kwa wakati mmoja.
“Hii itasaidia kupunguza gharama zinazotumika kwa nyakati mbili tofauti pamoja na kusaidia kupunguza mtikisiko wa amani nchini,”alisema.
Uchaguzi wa viongozi wa Serikali za mitaa hutangulia takriban mwaka mmoja kabla ya Uchaguzi Mkuu ambao huhusisha uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani.
Post a Comment