Header Ads

Mama Maria aipongeza serikali Daraja la Nyerere

MJANE wa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Maria Nyerere ametembelea Daraja la Nyerere linalounganisha eneo la Kigambaoni na Kurasini, Dar es Salaam na kuipongeza Serikali na wananchi wote wa Tanzania, kwa kufanikisha ujenzi wa daraja hilo kubwa na la kisasa kwa nchi za Afrika ya Mashariki na Kati.
Mama Maria aliyeongozana na mwanawe, Makongoro Nyerere alisema kukamilika kwa daraja hilo ambalo ujenzi wake umegharimu Sh bilioni 254.12, kumekamilisha mpango wa miaka mingi ulioanzishwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyekuwa na nia ya kujenga daraja katika eneo hilo la mkondo wa bahari, lakini kwa sababu ya ufinyu wa bajeti haikuwezekana.
Aidha, alimshukuru Rais John Magufuli kwa kuamua daraja hilo liitwe Daraja la Nyerere kwa heshimu ya Baba wa Taifa; na alibainisha kuwa uamuzi huo, utaviwezesha vizazi vijavyo kutambua juhudi zilizofanywa na mumewe katika ujenzi wa nchi.
“Mimi ninamshukuru sana Rais John Magufuli kwa maana ilikuwa lipewe jina lake, lakini yeye Mungu akamjalia akasema kwamba hapana, tukumbuke tulikotoka, kwa hiyo najisikia vizuri sana, na familia nayo inajisikia vizuri sana, lakini zaidi na Watanzania wanajisikia vizuri sana, kwa maana watakuwa wanaulizana Nyerere alikuwa ni nani?” alisisitiza Mama Maria.
Daraja la Nyerere lenye urefu wa meta 680, upana wa meta 32, njia sita za magari na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 2.5, lilifunguliwa na Dk Magufuli wiki moja iliyopita na linakuwa kiunganishi muhimu kati ya Kigamboni na katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
CHANZO:HABARI LEO

No comments