MAJAMBAZI YAUA WAWILI MKOANI GEITA
Watu 2 wameuawa kwa kupigwa na majambazi waliokuwa wamevamia katika baa inayofahamika kwa jina la High way pub iliyoko mtaa wa Mwatulole kata ya Buhalahala mkoani Geita.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo mratibu mwandamizi wa polisi Isack Msengi amesema kuwa tukio hilo limegunduliwa na msimamizi wa ulinzi wa kampuni ya Mara Security Didas John alipokuwa akikagua lindo baada ya kufika kazini mapema hii leo ndipo alipogundua kuuawa kwa watu hao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mratibu mwandamizi huyo inadaiwa kuwa majambazi hao walianza kumuua mlinzi wa baa hiyo bw, Yusuph Kilanga 38 mkazi wa Kivukoni kwa kumpiga na kitu kizito kichwani na baadae kuvunja dirisha la kaunta na kumuua msimamizi wa baa hiyo Jermiah Elias 19 mkazi wa Mwatulole kisha kumuingiza ndani alipokuwa amelala .
Baada ya kufanya mauaji hayo majambazi hao walichukua pesa kiasi cha sh. laki 4 zilizokuwa kaunta na baadae kuvunja duka la sementi lililopo jirani na eneo hilo na kuiba kiasi cha shilingi milioni 1, kisha kutokomea nazo kusikojulikana.
Katika eneo la tukio kumepatikana Msumeno mmoja mdogo na Fyekeo moja ambapo hadi sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa na polisi na kwamba jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi zaidi ili kuwabaini wahusika wa mauaji hayo.
Post a Comment