Header Ads

IDARA ZA TAMISEMI ZAONGOZA KWA RUSHWA MKOANI MWANZA.

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rusha Mkoani Mwanza (Pichani) Mhandisi Ernest Makale, leo ametoa taarifa ya Utendaji kazi wa taasisi hiyo mbele ya Wanahabari katika kipindi cha robo mwaka (Januari hadi Machi) mwaka huu.

Katika taarifa hiyo, Mhandisi Makale amebainisha kuwa Takukuru imepokea jumla ya malalamiko 45 yanayohusiana na vitendo vya rushwa kutoka kwa wananchi ambapo katika malalamiko hayo, 27 yameelekezwa kwa watumishi wa idara za Serikali za Mitaa TAMISEMI hiyo ikiwa ni sawa na asilimia 60. Kati ya malalamiko hayo 27, malalamiko 13 yameelekezwa katika idara ya ardhi.

Amesema idara zinazofuata kwa kulalamikiwa ni Mahakama yenye malalamiko tisa, polisi malalamiko sita na idara ya afya malalamiko matatu.

Mhandisi Makale amesema kesi 33 zinaendelea Mahakamani kutokana na vitendo vya rushwa Mkoani Mwanza huku kesi sita zikiwa ni mpya katika kipindi cha miezi mitatu na nyingine zikiwa katika upelelezi.

Amesema hatua zilizochukuliwa na Takukuru ni pamoja na kuwafikisha mahakamani watumishi waliolalamikiwa ambao ni Jesca Tongora ambae ni afisa ardhi Manispaa ya Ilemela, aliekuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela Henry Mtinda Matata, aliekuwa mhandisi Manispaa ya Ilemela Justine Lukaza, Mfanyabiashara Hemed Hamad aliehusika na kutoa zabuni ya kutoza ushuru katika kituo cha mabasi cha Buzuruga, Masoud Ramadhan na Arnold Massawe waliogushi vyeti na kujipatia ajira katika Mamlaka ya Maji taka na maji taka MWAUASA.

Wengine ni Zabron Marwa ambae ni afisa ugavi halmashauri ya Misungwi, Dr.Patrick Mwidunda aliekuwa DMO Halmashauri ya Magu, Yusuph Kaijage ambae ni afisa mifugo halmashauri ya Misungwi,  Masalu Kangalukwi na Amon Shija ambao ni wauguzi wa Hospital ya Wilaya Misungwi.

Katika Kipindi hicho cha miezi mitatu, Takukuru Mkoani Mwanza imeokoa kiasi cha shilingi Milioni 92 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara na hadi uchunguzi unafanyika pesa hiyo ilikuwa imeanza kutumika huku kazi ikiwa haijazaza ambapo Takukuru iliagiza fedha hizo kurejeshwa hazina. Pia Takukuru Mkoani Mwanza imefanya dhibiti 11 za vitendo vya rushwa, kuzuia warsha nane zilizokuwa na harufu ya rushwa.

Aidha Mhandisi Makale ametoa rai kwa wananchi na viongozi kutoa ushirikiano wao katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa ikiwemo kuwafichua wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo. 

Amezitaka halmashauri zote Mkoani Mwanza kufanya kazi kwa uadilifu na kwamba Takukuru inaendelea na uchunguzi wake dhidi ya watumishi hewa ambapo hadi sasa mbali na Takukuru imebaini watumishi hewa Watano katika halmashauri ya Jiji la Mwanza, ikiwa ni idadi iliyo nje na waliotangazwa na mkuu wa Mkoa wa Mwanza hivi karibuni.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rusha Mkoani Mwanza Mhandisi Ernest Makale, leo akitoa taarifa ya Utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa Wanahabari katika kipindi cha robo mwaka (Januari hadi Machi) mwaka huu.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rusha Mkoani Mwanza Mhandisi Ernest Makale, leo akitoa taarifa ya Utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa Wanahabari katika kipindi cha robo mwaka (Januari hadi Machi) mwaka huu.
Mhariri wa gazeti la Mtanzania Kanda ya Ziwa akiuliza swali kwa Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza.

No comments