WATUMISHI HEWA ZAIDI YA 100 WAGUNDULIKA KIGOMA
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Emanuel Maganga amewataka wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wote waliopo katika halmashauri zote kutaja kiasi cha fedha kilichotumika kuwalipa mishahara watumishi hewa 169 kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Akiongea na waandishi wa habari, Brigedia Jenerali Emanuel Maganga alisema kuwa agizo hilo ni kufuatia agizo la Mheshimwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli la kufanya uhakiki wa watumishi katika halmashauri zote ili kuwabaini watumishi hewa wanaolipwa mishahara kinyume na utaratibu za utumishi.
Alisema katika hao watumishi hewa 169 waliowabainika wapo ambao walishafukuzwa kazi, wapo ambao wameshafariki na wengine hawana sifa za kuwa watumishi wa umma.
Mhe. Maganga alisema kuwa suala la kuwa na wafanyakazi hewa ni wizi ambao hauwezi kuvumilika na wizi wa kuibia wanyonge hauwezi kuvumilika.
"Hakuna anayeweza kuvumilia wizi wa waziwazi kiasi hiki unaofanywa na baadhi ya watumishi wasiowaaminifu, wale wote watakaobainika wajiandae kwani hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao"Alisema Maganga.
Alisema kuwa fedha walizokuwa wakilipwa watumishi hao hewa kwaajili ya mishahara zinatakiwa kurudi zote, pia wakurugenzi wawafute watumishi hao hewa kwenye orodha ya malipo.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa sasa hivi katika serekali hii ya awamu ya tano hakuna kufanya kazi kwa mazoea.
Alizitaja halmashauri zenye watumishi hewa kuwa ni halmashauri ya kasulu watumishi 78,halmashauri ya Kigoma 23,Manispaa ya Kigoma Ujiji 29,halmashauri ya Buhigwe 11,Uvinza 19,kibondo 5,ofisi ya Mkuu wa Mkoa 4 na halmashauri ya Kakonko hakuna mtumishi hewa.
Post a Comment