Header Ads

Watakaopoteza watoto kizembe kukiona

                                                                       msemaji wa jeshi la polisi Advera Bulimba
POLISI imesema itawajibisha mzazi ama mlezi yeyote atakayeshindwa kutunza mtoto wake na kusababisha kupotea au kupata madhara katika kipindi hiki cha kusherehekea Sikukuu ya Pasaka ambayo inaadhimishwa kuanzia leo.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba (pichani), alitoa hadhari hiyo jana kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari na kuwataka wananchi kuwa makini na suala la ulinzi na usalama wa maisha na mali katika kusherehekea.
“Polisi haitasita kumwajibisha mzazi ama mlezi yeyote atakayeshindwa kutunza mtoto wake na kusababisha mtoto huyo kupotea au kupata madhara,” alisema Bulimba. Aliwataka wananchi wote kuwa wepesi katika kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vyovyote vya uhalifu katika maeneo yao ya makazi ama maeneo ya biashara.
Alikumbusha namba za simu za Polisi endapo mwananchi atakuwa na taarifa kuwa ni 111 au 112. “Tunapoelekea kipindi hiki cha sikukuu ya Pasaka ambayo inaanza (leo) Ijumaa Kuu, Jeshi la Polisi nchini, linatoa tahadhari kwa wananchi, kuwa makini katika suala zima la ulinzi na usalama wa maisha na mali zao,” alisema.
Alisema, katika kipindi cha sikukuu baadhi ya watu hupenda kutumia fursa hiyo kufanya vitendo vya uhalifu. Hata hivyo, alisema Polisi imejipanga vizuri kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika mikoa yote kuhakikisha kwamba hakuna vitendo vya uhalifu vitakavyojitokeza na pale vitakapojitokeza vitadhibitiwa kwa haraka.
Alisema, ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote, yakiwemo ya ibada, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu. Vilevile, jeshi hilo limetaka wananchi kuwa makini na watu wanaojipatia kipato kwa njia za utapeli kwa kutumia simu na mitandao.
“Mtu yeyote asikubali kutaja taarifa zake binafsi kwa asiyemjua, mfano kutaja namba ya siri ya akaunti anayotumia kuhifadhia pesa katika simu, ama kutuma pesa kwa mtu ambaye huna uhakika naye,” alisisitiza.
Wakati huo huo, msemaji huyo wa Polisi alihadharisha watumiaji wa barabara kwa kuwataka kuzingatia sheria za usalama barabarani. Alitaka madereva wa magari na pikipiki, kuepuka kujaza watu kupita kiasi, kubeba mishikaki, kwenda mwendo kasi, kutumia vilevi pamoja na kupiga honi hovyo.

No comments