Header Ads

Wamiliki wa Magari 213 Matatani..... TRA Yatoa Siku 4 Wajitokeze Kulipa Kodi Haraka




MAGARI 213 yanafuatiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya kubainika yameingizwa nchini bila kulipiwa kodi na watu binafsi pamoja na taasisi mbalimbali zikiwemo za dini.

Miongoni mwa magari hayo, yamo yaliyoingizwa kwa misamaha ya Kituo cha Uwekezaji (TIC) ambayo (misamaha) imetajwa kutumika isivyo.

Mamlaka imesema inafuatilia kuhakikisha wahusika sanjari na waliosaidia ukwepaji huo wa kodi, wanachukuliwa hatua.

TRA imetaja majina na taasisi zinazohusika na uingizaji magari hayo, kupitia matangazo kwa vyombo vya habari na imetoa siku nne wajitokeze kulipia ushuru kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa.

Ukaguzi uliofanywa na mamlaka, ndiyo umebaini kuwepo kwa magari hayo yaliyoingizwa nchini na kusajiliwa bila kufuata taratibu za forodha hivyo kuyafanya yamilikiwe bila kulipiwa kodi stahili.

Orodha ya magari 213 na namba za usajili, mmiliki na aina ya gari imetolewa katika vyombo vya habari na mamlaka hiyo imewataka wahusika wajitokeze haraka kulipia gharama hizo.

Baadhi ya kampuni, taasisi na watu binafsi, wameingiza magari zaidi ya moja.

Miongoni mwa taasisi zilizotajwa kwenye orodha hiyo zenye magari zaidi ya moja ni JM Hauliers Limited (26), Al-Jabri Co Ltd (16) na Kampuni ya Dhandho Road Hawlage iliyoingiza 18.

Kampuni nyingine na idadi ya magari yaliyoingizwa kwenye mabano ni Bamboo Rock Limited (7) na Dayosisi ya Musoma, ambayo hata hivyo haikufafanuliwa ni ya madhehebu gani ya dini, imeingiza magari manane.

Wengine ni Fai Limited (3), Nam Transport Company (6), Neni Enterprises (2) na Relief Partner International yenye magari matatu.

Kwa upande wa watu binafsi wenye magari zaidi ya moja yaliyoingizwa bila kulipia ushuru ni pamoja na Aloyce Kajijira (6), Mohamed Masoud (5), Mwesige Rwiza (5), Nassor Zakaria (3), Rumishaeli Shoo (3), Ruwaida Ally (4) Simon Mehi (2), Yahya Hilal (5) na Zahor Issa mwenye magari matatu.

Wapewa siku nne 
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo aliwataka wamiliki wa magari yaliyoorodheshwa kufika katika ofisi zilizo karibu, wafanyiwe uhakiki walipe ushuru stahiki kabla ya Machi 12 mwaka huu.

Alisema baada ya tarehe hiyo, TRA itachukua hatua ya kufuatilia magari hayo na kuyakamata.

Alisema ufuatiliaji wa magari yaliyoingizwa nchini bila kulipiwa ushuru ni endelevu.

Waliouziwa matatani 
Akizungumzia watakaokuwa wameuziwa magari hayo bila kufahamu kama yalitolewa bila kulipiwa kodi stahili, Kayombo alisema pia wanatakiwa kujitokeza.

Alisema walioyanunua magari hayo, ambayo namba zake zimeoneshwa, wanapaswa kujitokeza wapigiwe hesabu, walipe kiasi kinachodaiwa na mamlaka.

Kwa mujibu wa Kayombo, watakapofika katika ofisi za TRA, zitafanyika taratibu kuangali jinsi ya kulipa, kwani yapo magari ambayo hayakulipiwa kabisa au yamelipiwa kidogo kutokana na kufanya udanganyifu katika malipo.

Waliosaidia ukwepaji kodi 
Hata hivyo, Kayombo alisema baada ya kulipa gharama hizo, hatua nyingine zitachukuliwa.

Hatua hizo za kisheria, zitahusu waliopitisha magari hayo na waliosaidia katika kufanya udanganyifu wa kulipa kodi stahiki kwa magari hayo.


No comments