Header Ads

Shahidi wa Lembeli atinga kortini na mzigo wa masufuria ......Mawakili wajitoa kesi ya kupinga matokeo ya ubunge Jimbo la Kyerwa


Shahidi wa tatu wa mlalamikaji, James Lembeli katika kesi ya kupinga matokeo ya ubunge yaliyompa ushindi Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Jumanne Kishimba (CCM) jana alitinga Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga akiwa na mzigo wa masufuria, akidai alipewa kwa ajili ya kumpigia mgombea ubunge wa CCM. 

Mbele ya Jaji Moses Mzuna anayesikiliza shauri hilo, Cesilia Gregory wa Nyahanga mjini Kahama alikiri kupokea zawadi ya masufuria hayo kutoka kwa Wakala wa Kishimba ili ampigie kura. 

Gregory alidai Oktoba 19, 2015, Kikundi cha Amani waliitwa nyumbani kwa Hamad Hilal na kumkuta Ezra Machogu, ambaye alikuwa ni Wakala wa Kishimba akigawa masufuria yalitolewa kwa ajili ya kumuombea kura mgombea ubunge wa CCM. 

Hata hivyo, kulitokea mvutano baada ya Wakili wa Kishimba, Antony Nansimire kumtaka shahidi kuwataja wanakikundi 20 ambao walipewa masufuria hayo, hivyo kuwataja 22 na kwamba ongezeko hilo lilisababishwa na baadhi ya wanaume waliojiunga kuhamasisha utafutaji wapiga kura wa Kishimba. 

Wakati huohuo, mawakili wa mdai katika shauri la kupinga matokeo ya ubunge Jimbo la Kyerwa mkoani Kagera, Benedicto Mutungirehi wamejitoa. 

Hatua hiyo ilifuatia makosa ya kisheria yaliyobainishwa katika hati ya kiapo cha shahidi wa pili, Pastory Bagambila ambaye tayari alikuwa mbele ya Mahakama kutoa ushahidi wake. 

Baada ya kubaini makosa hayo, Wakili Erasto aliiomba Mahakama kumuondoa shahidi huyo kutoka kwenye orodha ya mashahidi kabla ya kutoa ombi la kujadiliana kwa muda na mteja wake. 

Hata shahidi wa tatu, Alistides Boniface alipoitwa naye hati yake ya kiapo ilibainika kuwa na kasoro za kisheria, hali iliyomtia hofu Wakili Erasto kuwa yawezekana viapo vya mashahidi wote 36 vilivyowasilishwa vina kasoro. 

Kabla ya kujitoa, wakili Erasto alimuomba Jaji Maisario Munisi anayesikiliza shauri hilo, kuahirisha kwa muda ili wajadiliane na mteja wao. 

Waliporejea mahakamani baada ya dakika 30, Wakili Erasto alimweleza Jaji Munisi kuwa wanaomba kujitoa kwa maelekezo ya mteja wao. 

Kutokana na hali hiyo, Mutungirehi aliiomba Mahakama kumpa muda kutafuta wakili, ombi lililokubaliwa na Jaji Munisi na kuiahirisha hadi Machi 22.

Mbunge wa sasa wa jimbo hilo kupitia CCM, Innocent Bilakwate anawakilishwa na Wakili Peter Matete.

Baadhi ya maombi yake ya msingi, Mutungurehi anadai kulikuwapo na ukiukwaji sheria, taratibu na kanuni katika kuhesabu kura na kudai kulitawaliwa na usiri bila kumhusisha.

No comments